Wainaina Anthony Njoroge amshukuru Mungu na wakazi wa Kieni

Wainaina Anthony Njoroge amshukuru Mungu na wakazi wa Kieni

NA SAMMY WAWERU

Wainaina Anthony Njoroge ndiye anasubiri kuapishwa awe mbunge mpya wa Kieni baada ya kuibuka mshindi kwa kuzoa kura 45,371 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022.

Mfanyabiashara huyo aliyewania ubunge kwa tiketi ya United Democratic Alliance (UDA) alimenyana na mpinzani wake, Kanini Kega aliyemfuata kwa kuzoa kura 25, 02.

Bw Kega, mbunge anayeondoka aliwania kutetea wadhifa wake kwa chama cha Jubilee.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta, alikuwa anasaka awamu ya tatu kuwa bungeni.

Shughuli ya kujumlisha kura na kutoa matokeo ilikamilika Alhamisi jioni Bw Wainaina akiridhia ushindi wake.

“Ninamshukuru Mungu kwa ushindi huu, familia na wenyeji Kieni kwa kuniamini na kunipa ushindi,” Bw Wainaina akasema baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi kutoka kwa afisa msimamizi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), eneobunge hilo, Bw David Mbui.

Afisa Msimamizi wa Kituo cha Kujumlisha Kura Kieni Bw David Mbui akitangaza ushindi wa Wainaina Anthony Nioroge. PICHA | SAMMY WAWERU

Akionekana akiwa mchangamfu baada ya kutangazwa mshindi katika Shule ya Upili ya Mweiga, ambayo ilikuwa kituo kikuu cha kujumlisha kura, Wainaina aliahidi kuhudumia wakazi wa Kieni.

“Nimejitolea kuwafanyia kazi tuboreshe eneo letu,” akasema.

Bw Mbui, afisa wa IEBC, alieleza kufurahishwa kwake na zoezi zima la uchaguzi Kieni akisema lilisheheni amani.

“Kieni ni kati ya maeneo nchini ambayo shughuli ya uchaguzi iliendeshwa kwa utulivu na amani,” afisa huyo akasema.

Afisa huyo, makarani wa IEBC na maafisa wa usalama walitangamana na wanahabari na wapigakura kwa karibu, ushirikiano uliosaidia kuendesha upigaji kura kwa njia ya amani.

Bw Wainaina Anthony Njoroge akitangamana na maajenti wake katika Shule ya Upili ya Mweiga, ambayo ilikuwa kituo kikuu cha kujumlisha kura. PICHA | SAMMY WAWERU

Kisa kilichoshangaza na kuzua ucheshi katika Shule ya Mweiga, ni karani aliyeangua kilio, akapiga nduru akiririkwa na machozi wakati akiwasilisha masanduku yenye kura kukaguliwa.

Uchunguzi wa polisi ulibaini alikuwa ametumia kileo, maafisa hao wakimsamehe.

“Huyu ni kijana – karani ambaye amelewa… Atajielewa pombe ikimwisha,” akasema mmoja wa maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria.

Aliponea tundu la sindano kuwekwa seli, maafisa hao wakimsamehe.

Wawaniani wengine kiti cha ubunge Kieni, walikuwa: Martin Wachira Maina aliyekwagura kura 2,398, Muchire Stephene (651) na Wanjau Jackson 489.

Vilevile, Kinyua Jane Wairimu alikuwa debeni akizoa kura 477 na David Mwangi 376.

Baada ya kupokezwa cheti cha ushindi, Bw Wainaina alifululiza hadi Mweiga Mjini, ambapo alitangamana na wapigakura kuwashukuru.

Bw Kega, Jumatano alitangaza kukubali kushindwa kuhifadhi kiti chake.

  • Tags

You can share this post!

Amri waliozua hofu kura zikijumlishwa Mavoko wakamatwe

KIKOLEZO: Penzi lakubali mabosslady!

T L