Habari za Kitaifa

Waislamu 5,000 kufurahia msaada wa chakula Ramadhan

February 26th, 2024 1 min read

NA CECIL ODONGO

RAMADHAN ya mwaka huu inapokaribia, Zakat Kenya na Benki ya Premier, Jumapili, Februari 25, 2024 ziliandaa matambezi ya kuchangisha Sh30 milioni kugharimia Iftar kwa zaidi ya Waislamu 5,000 wakati wa mwezi huo mtukufu.

Mwaka huu, Ramadhan ambayo ni Nguzo ya Nne ya Dini ya Kiislamu, inatarajiwa kuanza Machi 10 hadi Aprili 9 kulingana na mwandamo wa mwezi.

Ramadhan ni mwezi wa tisa kwenye kalenda ya Waislamu ambapo Waislamu hufunga kutokana na kuchomoza na kutua kwa jua.

Jumapili, Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Premier Osman Duale na Naibu Mkurugenzi wa Zakat Kenya, Abdi Shakur waliwaongoza Wakenya na Waislamu katika matembezi yaliyolenga kupata pesa za kulisha maskini Nairobi na maeneo mengine.

Matembezi hayo yenye kauli mbiu ‘Sisi Ni Mamoja, Matembezi ya Hiari ya Iftar’ yalianzia katika Mskiti wa Adams Arcade na kuishia Sir Ali Muslim Club mtaani Eastleigh, Nairobi.

Pesa ambazo zilichangishwa, zitatumika kununua chakula ambacho kitasambazwa Nairobi na maeneo ya karibu Machi 10, 2024.

Vyakula hivyo vitatolewa kwa Waislamu masikini kabla ya kuanza kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhan.

“Tunataka kupunguza changamoto ambazo zinakabili ndugu zetu Waislamu wakati wa Ramadhan. Wazo hili ni la kuyainua maisha ya Waislamu wakati wa Ramadhan,” akasema Bw Osman.

Bw Mohammed alisema chakula ambacho kilisambazwa kitasaidia familia kumakinikia mfungo. Mpango huu wa kusaidia Waislamu wakati wa Ramadhan, umekuwa ukiendelea kwa miaka saba na lengo lake kuu ni kuifaa jamii.