Habari Mseto

Waislamu kuingiza tende bila kulipia ushuru

February 1st, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Ulinzi Aden Duale ameishukuru serikali ya Rais William Ruto kwa kuwaondolea Waislamu hitaji la kulipia ushuru tende watakazoingiza nchini wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Kwenye taarifa mnamo Jumatano, Bw Duale alielezea furaha yake kwa Rais Ruto kufuatia hatua hiyo.

“Hatua hiyo inaashiria na kuthibitisha imani yetu katika taifa moja lenye dini tofauti, kama ilivyo kwenye Katiba,” akasema.

Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SCKM) lilikuwa limemwandikia barua waziri, likimrai kuwasaidia wafuasi wa dini hiyo kuondolewa ulipaji ushuru na serikali, wanapoagiza bidhaa wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Ombi hilo liliwasilishwa kupitia Katibu Mkuu wa baraza hilo, Abdullahi Salat, kwenye barua aliyoandika Januari 25, 2024.

Kutokana na hatua hiyo, Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u, alitangaza kwamba badala yake, serikali italipia ushuru bidhaa zitakazoagizwa na Waislamu wakati wa mfungo huo.

“Katika kuonyesha uungwaji mkono kwa Jamii ya Kiislamu, serikali imeagiza kwamba bidhaa zitakazoagizwa wakati wa mfungo wa Ramadhan hazitatozwa ushuru wowote,” akasema.

Mfungo huo utadumu kati ya Machi 10, 2024, na Aprili 4, 2024, ingawa tarehe zinaweka kubadilika kutegemea mwandamo wa mwezi. Hata hivyo, serikali ilisema kuwa Waislamu hawatatozwa ushuru kwa bidhaa watakazoagiza kati ya Machi 1, 2024, na Aprili 20, 2024.

Mamlaka ya Kukusanya Ushuru Kenya (KRA) pia ilithibitisha hatua hiyo kupitia Kaimu Naibu Kamishna wa Sera na Masuala ya Kimataifa, Bi Lucy Ng’ang’a.

“Muda wa bidhaa hizo kutotozwa ushuru utakamilika Aprili 20, 2024. Bidhaa zitakazoagizwa baada ya hapo zitatozwa ushuru kama kawaida,” akasema kwenye taarifa Jumatatu.