Habari

Waislamu kuswali na kusherehekea Eid al-Fitr kesho Jumapili

May 23rd, 2020 2 min read

MISHI GONGO na MOHAMED AHMED

KADHI Mkuu nchini Ahmed Muhdhar amewatangazia Waislamu waswali na kusherehekea Eid al-Fitr kesho Jumapili baada ya kukamilika mwezi wa Ramadhan.

Sheikh Muhdhar amesema mwezi umeonekana eneo la Lamu.

“Nimepata habari kuwa mwezi umeonekana Lamu na nina furaha kutangaza kuwa kesho Jumapili tutasherekea Idi. Ni himizo langu kuwa Waislamu wenzangu wanafuata maagizo kwa sababu ya lile janga ambalo tuko nalo la Covid-19,” amesema Sheikh Muhdhar.

Wakati huo huo, amepinga kuwa mwezi ulionekana Ijumaa na kusema kuwa leo Jumamosi ndiyo imekuwa siku mwafaka ya kutazama mwezi.

Alisema kuwa kulingana na wasomi, haiwezekani kuwa mwezi ulionekana Ijumaa.

“Leo (Jumamosi) ndiyo siku ya 29 na ndiyo maana tumeangalia mwezi. Mwezi huwa ni siku 29 ama 30 an tumeona kuwa tumetimiza hilo. Tunashukuru hali ya anga iko wazi,” ameeleza.

Ameyasema hayo akiwa mjini Mombasa ambako waumini wengi wa dini hiyo Jumamosi mchana hadi jioni wameonekana katika masoko mbalimbali wakinunua bidhaa za maandalizi ya sikukuu hiyo.

Wengi wameonekana wakinunua vyakula katika soko la Kongowea na Mwembe Kuku mjini humo.

Tangu kufungwa kwa soko la Marikiti kwa kuhofia kusambaa kwa virusi vya corona, waliokuwa wakiuza bidhaa katika soko hilo walihamia Mwembe Kuku kuendeleza biashara zao.

Akizungumza na Taifa Leo katika soko la Mwembe Kuku Bi Mariam Juma aliyekuwa ameandamana na watoto wake watatu kuwanunulia nguo, amelalama kwamba bidhaa zinauzwa bei ghali.

“Bidhaa zimepanda maradufu; suruali tulizonunua Sh1,200 sasa hivi ni Sh2,000,” amesema mzazi huyo.

Alikuwa amevalia maski.

Muuzaji mmoja hapo sokoni aliyezungumza na wanahabari ni Bw Rashid Ali.

Hali ilikuwa vivyo hivyo katika soko la Kongowea.

Walioadhimisha Eid al-Fitr leo Jumamosi pia wameonekana wakitembea nje angaa kufurahia.

Bi Aisha Yusuf amesema ni ada kwa familia yake kutembelea mamake kila siku ya Idi.

Mazoea yangu siku za kawaida huwa ni kutembelea jamaa zangu.

“Huwa siku ya kwanza nazuru familia ya mume wangu ama yangu kisha siku ya pili nawapeleka watoto katika sehemu za burudani. Kufuatia kufungwa sehemu nyingi za burudani nimeamua kutembelea jamaa na marafiki zangu,” akasema.

Alisisitiza kuwa sikukuu hiyo haitakuwa na maana sana kwake iwapo hatatembelea jamaa zake ili kuwajulia hali.

Wauzaji wa mbuzi sokoni Kikowani, Mombasa ambako bei ya mifugo hiyo imepanda wakati huu wa maandalizi ya Eid al-Fitr Mei 23, 2020. Picha/ Kevin Odit