Habari

Waislamu sasa watofautiana kuhusu BBI

November 23rd, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

VIONGOZI wa dini ya Kiislamu wamegawanyika kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Hii ni baada ya Mwenyekiti wa kitaifa wa Baraza la Kitaifa la Ushauri kwa Waislamu (KEMNAC), Sheikh Juma Ngao na viongozi wengine wa kidini kutoka eneo la Pwani kupinga kauli ya Baraza Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM).

Mnamo Jumapili, Supkem ilitangaza kuwa haiungi mkono ripoti hiyo na kudai yaliyomo katika ripoti hiyo ni kinyume cha yale waliotarajia. Viongozi wa Supkem walisema ripoti ya BBI jinsi ilivyo kwa sasa ni hatari kwa ugatuzi na itarudisha nyumaufanisi uliopatikana chini ya katiba ya 2010.

Hata hivyo, Kemnac ilisema Supkem ilifikia uwamuzi huo bila kujumuisha makundi mengine ya kidini hivyo hawapaswi kujumuisha Waisilamu wote katika uamuzi wao.

“Tuko na vyama 250 vinavyowakilisha Waislamu nchini, waliotia sahihi kauli ya Supkem ni vyama vinne tu hivyo wanapaswa kusema hayo ni maoni yao na si ya Waislamu wa Kenya nzima,” akasema Sheikh Ngao kwenye kikao cha wanahabari Mombasa.

Bw Ngao alisema baraza la Kemnac linaunga mkono ripoti ya BBI japo alitoa mapendekezo ambayo alitaka yaongezwe.

Alisema sasa ni wakati muafaka wa kubadili baadhi ya vipengee vya katiba kwa maslahi ya Wakenya wote. Alizungumzia suala la dhuluma za ardhi katika eneo la Pwani, kuuawa kwa watu kiholela, kufufuliwa kwa viwanda mbali mbali eneo la Pwani, na mapato ya bandari za Lamu na Mombasa.