Waislamu waenda Saudia kwa Umrah

Waislamu waenda Saudia kwa Umrah

Na CECIL ODONGO

BARAZA Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM) limeshukuru serikali ya Saudi Arabia kwa kufungua baadhi ya maeneo matakatifu ya kuabudu kwenye mji wa Mecca huku mahujaji 20 wakisafiri kushiriki ibada ya Umrah hapo jana.

Safari hiyo inawadia mwaka mmoja unusu tangu Saudia iwaweke raia wa mataifa ya nje marufuku ya kuingia nchini humo kutokana na kupanda kwa maambukizi ya corona.

Mnamo Jumapili, serikali ya Saudia hata hivyo ililegeza msimamo na ikafungua baadhi ya maeneo takatifu ya kuswali jijini Mecca.

Maeneo hayo yalifungwa mnamo Februari mwaka huu na ibada kuzimwa kutokana na corona huku kufunguliwa kwao kukihusishwa na kupungua kwa maambukizi ya janga hilo.

Umrah ni ibada ya Kiislamu ambapo muumini huzuru Mecca wakati wowote na kutia dua. Ni tofauti na Hajj ambayo ni ibada inayofanyika mara moja kwa mwaka na ni kati ya nguzo tano za Kiislamu.

Hapo jana, Mshirikishi wa Supkem Kaskazini Mashariki mwa Bonde la Ufa Sheikh Adan Yunis ambaye aliratibisha safari ya mahujaji hao 20, alithibitisha kuwa wote walikuwa wamepokea chanjo mara mbili na walikuwa na vyeti vya kuthibitisha upokeaji wa chanjo kutoka vituo vinavyotambulika vya kiafya.

Sheikh Yunis pia alishukuru serikali za Kenya na Saudia akiwemo Mfalme wa nchi hiyo ya Kiarabu Salman Bin Abdulaziz Al Saud, mwanawe mfalme Bin Salman na ubalozi wa Kenya nchini Saudia kwa kufanikisha safari hiyo ya mahujaji.

“Waislamu wengi husafiri hadi Mecca kutekeleza ibada ya Umrah kando na ile ya Hajj ila hilo halijakuwa likifanyika baada ya safari za mahujaji wa nje kuzimwa. Tunashukuru serikali zote kwa sababu sasa kila moja yupo huru kusafiri na kutekeleza ibada ya Umrah,” akasema Sheikh Yunis.

“Pia nawaomba mahujaji waliosafiri wazingatie masharti yote yaliyowekwa na serikali ya Saudia kusaidia kupambana na janga la corona. Hii itasaidia kuhakikisha maeneo hayo matakatifu hayafungwi tena,” akaongeza.

Kufunguliwa kwa maeneo hayo matakatifu ya Ibada jijini Mecca ni afueni kwa Waislamu kutoka hapa nchini ambao wamekosa kushiriki hata Hajj kwa miaka miwili mfululuzo.

Mwaka huu ni raia 60,000 pekee wa Saudia walioruhusiwa kutekeleza ibada ya Hajj na nchi hiyo haikuwaruhusu mahujaji kutoka nje ya nchi.

Mwaka jana, Waislamu 10,000 pekee ndio walishiriki Hajj, hii ikiwa chini zaidi ya Mahujaji milioni 2.5 ambao walikuwa wakifika Mecca kabla ya ujio wa corona 2019.

You can share this post!

Serikali inavyokiuka Katiba kuacha raia wafe njaa

Mzozo wa DPP na DCI waanikwa na kesi ya mauaji ya Cohen