Waislamu walaani MUHURI kuajiri ‘mtetezi wa mashoga’

Waislamu walaani MUHURI kuajiri ‘mtetezi wa mashoga’

Na FARHIYA HUSSEIN

JAMII ya Waislamu nchini imeomba Baraza Kuu la Waislamu la Kenya (SUPKEM) liingilie kati kuhusu uamuzi wa shirika la Muslims for Human Rights (MUHURI) kuajiri Mkurugenzi Mkuu anayedaiwa kuwa mtetezi wa wapenzi wa jinsia moja.

Katika barua iliyoandikwa kwa Mwenyekiti wa MUHURI, Bw Khelef Khalifa, waumini wa dini ya Kiislamu walisema wamekerwa sana na hatua ya MUHURI.

“Sisi kama Waislamu wa Kaunti ya Mombasa na Kenya kwa jumla, tumehuzunishwa sana na hatua ya hivi majuzi ya kumwajiri mkurugenzi mkuu mpya katika MUHURI. Tunakashifu vikali uamuzi uliochukuliwa na bodi ya shirika hilo kumwajiri mtu anayeenda kinyume na maadili ya dini yetu,” barua hiyo ikasema.

Walalamishi walisema hawatakaa kimya na kukubali shirika linalotumia jina la Uislamu kuendeshwa kwa misingi ya itikadi ambazo zinaenda kinyume na mahitaji ya kidini.

“Hatua iliyochukuliwa inayonyesha wazi kwenda kinyume na mafunzo ya Kiislamu. Tunataka bodi iitishe kujiuzulu kwa mkurugenzi mkuu mpya mara moja,” barua hiyo ikazidi kusema.

Kufuatia hali hiyo, wanamtaka Bw Khalifa abadilishe jina la MUHURI ili likome kuhusishwa na Uislamu.Bila hilo, wametishia kuitisha maandamano ili kukemea wazi mienendo ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu.

Mapema mwezi huu, MUHURI ilitangaza kumwajiri Bi Marie Ramtu kuwa mkurugenzi mkuu mpya. Bi Ramtu aliwahi kufanya kazi katika shirika la kutetea haki za binadamu la Network of African National Human Rights Institution (NANHRI)

Aliwahi pia kuhudumu katika shirika la Church World Service, ambapo inasemekana alihudumu kulinda masilahi ya watu walio hatarini kudhulumiwa kingono au kijinsia.

You can share this post!

Hichilema aanza kazi kwa kishindo, atimua polisi na...

Polisi mpakani wapepeta corona kwa hongo ya Sh2,000