Habari za Kitaifa

Waislamu washauriwa kudumisha maadili

March 25th, 2024 1 min read

ABDULRAHMAN SHERIFF Na KARIM RAJAN

WAUMINI wa Kiislamu nchini Kenya wametakiwa kuzingatia mafundisho ya dini, wakihimizwa kwamba yanachangia pakubwa katika kujenga tabia ya mtu kimaadili.

Akizungumza wakati wa mashindano ya kuhifadhi Kuran katika uwanja wa Makadara mjini Mombasa, Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Abdulhalim Hussein alisema mafunzo ya dini yanayotolewa kwenye misikiti na madrassa yamesaidia pakubwa kurekebisha tabia za vijana.

Kadhi Sheikh ndiye alikuwa mgeni wa heshima katika hafla hiyo.

“Mafunzo ya dini ya Kiislamu yamesaidia vijana kwa kiasi kikubwa kujiepusha na utumiaji dawa za kulevya na kushiriki kwenye magenge ya uhalifu ambayo yanachangia utovu wa usalama,” akasema Sheikh Hussein.

Aidha, Kadhi Mkuu amehimiza waumini kuutumia vyema mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kujishughulisha na ibada, kusoma Kuran kwa wingi na kuepukana na vitendo ambavyo vitawachochea kushiriki dhambi.

Sheikh Hussein pia amewataka Waislamu kuwekeza zaidi katika kuhifadhi na kusoma Kuran, akibainisha kuwa mafundisho ya kitabu hicho takatifu yanasaidia waumini kutekeleza maadili mema yanayotakikana kufuatwa katika shughuli za maisha ya kila siku.

Mashindano hayo ya siku tatu yamejumuisha wanafunzi kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Tanzania, Uganda, Somalia, Burundi, Congo, Rwanda na Zanzibar.

Wanafunzi waliwekwa katika vitengo vinne vya kuhifadhi juzuu tano, kumi, 20, na 30.

Katika mashindano hayo ya makala ya 20 yaliyotayarishwa na Muslim Mercy Youth (MMY), Yunus Masoud wa Markaz Aldaawa kutoka Ukunda aliibuka mshindi wa hapa nchini kwa kuhifadhi juzuu 30 na akatunukiwa Sh60, 000 na kifurushi cha kwenda kuhiji Mecca.