Habari Mseto

Waislamu wataka misikiti ifunguliwe Ramadhan

April 16th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

BARAZA la maimamu na wahubiri nchini (CIPK), limeiomba serikali kufungua misikiti na kupunguza saa za kafyu katika mwezi mtukufu wa Ramadhan ili kuwawezesha waumini kufanya ibada zao kama inavyotakiwa.

Serikali ilitoa amri ya kufungwa kwa misikiti kama njia moja ya kuhakikisha kuwa wanadhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Mombasa ni kaunti ya pili inayoongoza kwa idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini.

Wakizungumza katika kikao na wanahabari jana katika ukumbi wa Baluchi mjini Mombasa, viongozi hao walisema waumini pia wanahitaji muda jioni kutoa chakula kwa wasiojiweza katika jamii kama ilivyo ada katika mwezi huo.

Kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir na seneta wa Mombasa Mohammed Faki, kilikuwa ni cha kuwasilisha mapendekezo ya waumini wa dini ya Kiislamu wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao unatarajiwa kuanza baada juma lijalo.

Mkurugenzi wa baraza hilo Sheikh Khalifa Mohammed, alisema kafyu itanyima familia zisizojiweza kupata msaada usiku.

“Kuna wale wanategemea kufuturishwa na watu wengine, pia kuna wale wanaotegemea misikiti kupata chakula chao cha kila siku hivyo kufungwa kwa misikiti na kafyu kutawatatiza,” akasema Sheikh Khalifa.

Aidha, waliiomba serikali kuhusisha Maimamu katika ratiba ya kugawanya chakula kwa jamii zisizojiweza.

“Maimamu ni viungo muhimu katika jamii, kuhusishwa kwao kutahakikisha kuwa hakuna mtu anasazwa katika ratiba hiyo ya chakula,” akasema Imamu wa msikiti wa Jundani sheikh Aboud Mohammed