Habari za Kitaifa

Waislamu watofautiana kuhusu kuanza kwa mwezi wa Dhul Hijjah

June 7th, 2024 1 min read

NA FATUMA BUGU

KWA mara nyingine tena, waumini wa dini ya Kiislamu wametofautiana kuhusu kuandama kwa mwezi wa Dhul Hijjah.

Kadhi mkuu nchini Abdulhalim Hussein, tayari ametangaza kuwa siku kuu ya Eid ul-Adha itakuwa Juni 16.

“Tunathibitisha kuonekana kwa mwezi mjini Mecca mnamo Alhamisi na hivyo siku ya kwanza ya Mwezi wa Dhul Hijja itakuwa Ijumaa huku Siku ya Arafa ikitarajiwa kuwa Jumamosi, ” alisema Kadhi Mkuu.

Kauli hiyo inakinzana na ile ya Baraza la Fatwa Kenya pamoja na ushirikiano na Mamufti wa Afrika Mashariki ambapo walikiri kuwa kulingana na takwimu za hesabu ya mwezi, mwezi hauwezi kuandama siku ya Alhamisi Afrika nzima na hata sehemu nyingi ulimwenguni.

Kwa mujibu wa baadhi ya viongozi wa kidini, miaka yote nchini, Kadhi Mkuu ndiye anayepaswa kutangaza kuandama kwa mwezi.

“Kulingana na ufahamu wake, ni kuwa mwezi wa Ramadhan huangaliwa mwezi wa nyumbani, yaani kieneo, huku mwezi wa Dhul Hijjah ukitazamwa muandamo wa mwezi wa nje kulingana na mahusiano ya Ibada ya hajj,” alisema Sheikh Omar Buya, ambaye ni kiongozi wa kidini.

Tangazo rasmi la mwandamo wa mwezi wa Dhul Hijjah kwa hiyo lina umuhimu mkubwa kwa umma wa Kiislamu.

Ni wakati ambapo waumini wanaitwa kutazama anga kwa makini ili kuona mwezi mpevu wa kwanza, unaoashiria mwanzo wa mwezi mpya.

“Twawahimiza Waislamu wajitokeze kwa wingi kuangalia mwezi siku ya Ijumaa na kutoa taarifa kwa wahusika mara moja iwapo mwezi utaandama,” alisema Ahmad Badawy, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Fatwa Kenya.

Dhul Hijjah ni kimojawapo cha vipindi vitakatifu vya mwaka kwenye kalenda ya Kiislamu ambapo Siku 10 za mwanzo za Dhul Hijjah, wale ambao hawana uwezo wa kuhiji, hufanya ibada mbalimbali ikiwemo kufunga siku tisa za Dhul Hijjah. Waislamu husheherekea sikukuu ya Eid ul-Adha kwa kuchinja wanyama kama vile mbuzi, kondoo, ngamia na ng’ombe.