Habari

Waislamu wengi wajitokeza Ijumaa ya mwisho Ramadhani

May 31st, 2019 2 min read

Na MOHAMED AHMED

WAISLAMU wamejumuika katika misikiti mbalimbali humu nchini kwa ajili ya swala ya Ijumaa mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani huku wengi wakijiandaa kwa siku kuu ya Eid al-Fitr.

Wakati wa swala hiyo ya Ijumaa jijini Mombasa, Sheikh Mohammed Ali Rashid ambaye aliongoza hotuba ya swala hiyo alitoa mwito kwa waumini kuongeza kulisha maskini katika jamii ili ibada zao za funga ziweze kukubalika.

Mombasa ni jiji la pili kwa ukubwa nchini Kenya baada ya Nairobi ambalo ndilo jiji kuu na makao rasmi ya asasi nyingi za serikali kuu.

“Hizi ni siku za mwisho za mwezi huu wa Ramadhani, tayari leo (Ijumaa) tumekamilisha Ijumaa ya mwisho hivyo basi ni lazima tuongeze matendo mema ili tuweze kupokelewa kwa funga zetu na Mungu. Ili sote tuweze kusherehekea kwa pamoja, ni lazima wale walio nacho wasaidie wenzao ambao hawana,” akasema Sheikh Rashid baada ya swala hiyo katika msikiti wa Ummul Kulthum jijini Mombasa.

Baada ya kumalizika kwa swala hiyo, waumini wa dini hiyo waliliminika katika maeneo ya biashara eneo la Mombasa Mjini kwa ajili ya kununua bidhaa za matayarisho ya Eid al-Fitr.

Eid al-Fitr ni sherehe ya kukamilisha saumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na mwaka huu inatazamiwa kusherehekewa ama siku ya Jumanne au Jumatano ikitegemea kwa mwonekano wa mwezi. Mwezi wa Ramadhani unatazamiwa kumalizika siku ya Jumatatu ama Jumanne.

Ijumaa, wakazi wengi walifurika katika maeneo ya Marikiti, Majengo na Mji wa Kale kwa ajili ya kununua vitu ikiwemo nguo mpya na bidhaa za kutumika pale nyumbani.

Baadhi ya wanunuzi wamelalama bei za bidhaa zimepanda.

“Tumeshukuru mwezi unaenda kuisha salama lakini wakati huu tunapotaka kujitayarisha kwa ajili ya Eid al-Fitr tumepata wakati mgumu kwani bidhaa nyingi zimekuwa ghali mno,” akasema Suleiman Hashim, mmoja wa wanunuzi.

Kwingineko, katika pitapita za Taifa Leo baadhi ya misikiti imepakwa rangi ili iwe ya kuvutia zaidi ifikapo siku ya kukamilisha saumu – yaani Eid al-Fitr.

Swala hiyo ya Idi pia itatekelezwa katika viwanja vya wazi kama ilivyo ada ya waumini wa dini hiyo.