Bambika

Waithaka wa Jane: Mfalme wa ‘Mugithi’ asiyekunywa pombe

March 3rd, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

WAKATI mwanamuziki wa mtindo wa Mugithi, Salim Junior, alipofariki mnamo 2021, kifo chake bila shaka kilikuwa pigo kubwa kwa tasnia ya muziki huo katika ukanda wa Mlima Kenya.

Wengi walisema ingekuwa vigumu kwa pengo aliloliacha kujazwa, kwani uimbaji wake kwa kucheza gitaa moja (one man guitar), ulikuwa wa kipekee.

Yeye ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa mtindo huo wa muziki katika ukanda huo, kuanzia miaka ya 2000.

Kupitia mtindo huo, Salim alikuwa akiimba nyimbo za wanamuziki wa zamani wa lugha ya Gikuyu, kama vile John Ndichu, Joseph Kamaru, Musaimo, Ruguiti wa Njeeri kati ya wengine wengi.

Baada ya kifo chake, ni wanamuziki wachache sana waliopigiwa upatu kujaza nafasi yake, miongoni mwao wakiwa kakake, Mighty Salim.

Hata hivyo, malaika wa mauti hakuwaacha mashabiki wa ‘mugithi’ kutulia kwani mnamo 2021, Mighty Salim pia alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Vifo hivyo viwili vilikuwa pigo kubwa kwa tasnia ya muziki katika ukanda wa Mlima Kenya.

Hata hivyo, wakati wa janga la virusi vya corona (kati ya 2020 na 2021), kulichipuka barobaro mwingine, aliyewashtua wengi kutokana na weledi wake katika uchezaji gitaa na uimbaji wa nyimbo za wanamuziki wa enzi za kale.

Barobaro huyo ni mwanamuziki Waithaka wa Jane almaarufu kama ‘Karaiku Master’ miongoni mwa mashabiki wake.

Kwa sasa, mwanamuziki huyo amejijengea jina kama miongoni mwa wanamuziki maarufu sana katika eneo la Kati.

Waithaka, kwa jina halisi, John Waithaka Mwangi, ni mzaliwa wa Kaunti ya Murang’a.

Yeye ndiye kitindamimba kwenye familia ya watoto wanane—wavulana sita na wasichana wawili.

Tangu alipojitosa rasmi kwenye tasnia ya muziki wa ‘Mugithi’ kuanzia mwishoni mwa 2022, watu wengi wamemtaja kama ‘Salim Junior wa Kizazi cha Sasa’, kutokana na weledi wake mkubwa katika uchezaji gitaa.

Soma Pia: Mike Rua: Mimi ndiye ‘Big Daddy’ wa Mugithi wengine wakijiita wafalme

Hata hivyo, kinyume na wanamuziki wengi wa nyimbo za kidunia, Waithaka anasema kuwa yeye hanywi pombe, kwani amelelewa katika familia ya Kikristo.

“Hata ikiwa huwa naimba nyimbo za kidunia, nimelelewa kwa msingi wa dini ya Akorino. Ni msingi ulionjenga sana kimaadili. Hata ikiwa huwa ninawatumbuiza mashabiki wangu kwenye vilabu, huwa sinywi pombe,” akasema mwanamuziki huyo.

Kwa sasa, staa huyo anatamba kwa nyimbo kama ‘Karaiku’, ‘Wangechi’, ‘Kiunuhu’, na majuzi ‘Nyuumite Kuraaya’ – wimbo unaomaanisha ‘Nimetoka Mbali’.

Anasema huwa anazingatia sana maadili ya Kikristo, ikizingatiwa mamake ni mfuasi sugu wa dini ya Akorino. Marehemu babake alikuwa mhubiri.

“Umaarufu kamwe haujanibadilisha. Bado ninakumbuka nilikotoka. Tumelelewa kwa shida nyingi sana. Siwezi kujikwaa kimaadili kutokana na umaarufu nilio nao kwa sasa,” akasema.