Habari Mseto

WAITIKI: Watu 3,000 hawajachukua hatimiliki zao miaka 4 baadaye

March 20th, 2019 1 min read

Na MOHAMED AHMED

MAELFU ya hatimiliki za wakazi wa Waitiki bado hazijachukuliwa na wenyewe, miaka minne toka serikali ipeane stakabadhi hizo.

Stakabadhi hizo zimejaa kwenye afisi za ardhi jijini Mombasa huku rekodi ikionyesha kuwa hatimiliki 1, 750 bado hazijachukuliwa.

Rais Uhuru Kenyatta alipeana hatimiliki hizo Januari mwaka 2016 kwa wakazi hao eneo la Shikaadabu, Likoni.

Wakati wa kupeana hatimiliki hizo, Rais Kenyatta alisema kuwa wakazi hao watapaswa kulipa Sh182, 000 kila mmoja.

Hata hivyo, miezi mitatu baadaye, gavana wa Mombasa Hassan Joho alisema kuwa kaunti yake italipa pesa hizo.

Aidha baadaye mwaka huo, Bw Joho alibadilisha semi zake na kusema kuwa hatolipa tena pesa hizo. Matamshi hayo yalitokana na tofauti za kisiasa baina yake na Rais Kenyatta.

Hata hivyo, kuahidiwa kulipiwa kwa ada hiyo ndio mojawapo ya sababu ya hatimiliki hizo kutochukuliwa.

Mwenyekiti wa wakazi wa Waitiki Abdallah Fuad alisema kuwa wakazi hao wametatizika kwa muda na kupelekea hati hizo kuachwa katika afisi hizo.

“Wakazi hawataki kwenda kuchukuwa hatimiliki kwa sababu waliambiwa watalipiwa lakini baadaye wakageukwa na sasa malalamishi mengine ni kuhusiana na stakabadhi ambazo zipo na majina tofauti na ya wale wanayostahili kupata,” akasema Bw Fuad.

Kamishna wa Mombasa Evans Achoki alisema kuwa hatimiliki hizo za wakazi wa Waitiki ni miongoni mwa 3, 000 ambazo hazijachukuliwa na wakazi wa maeneo tofauti wa Mombasa baada ya serikali kutoa stakabadhi hizo.

Rikodi inaonyesha kuwa kuna hatimiliki 308 za wakazi wa eneo la Ziwa la Ngombe, 175 eneo la Mikanjuni na 178 za wakazi wa Majaoni.

Bw Achoki alisema kuwa stakabadhi hizo zitapelekwa kwenye afisi za chifu kwenye maeneo hayo ili kuruhusu wakazi kuzifikia hatimiliki hizo kwa wepesi.

“Kile nitawasihi ni kuwa musiuze hatimiliki hizo mtakapozipata. Hizi ni stakabadhi ambazo zitawasaidia nyinyi na vizazi vyenu,” akasema Bw Achoki.