Habari

Waititu aibuka na jipya

June 1st, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

GAVANA wa Kiambu, Ferdinand Waititu, Jumamosi ametoa onyo kuwa ikiwa kuna lolote baya litawatokea baadhi ya watu wa familia yake, basi wa kuulizwa watakuwa ni watu wanne.

“Watu hao ni aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo, Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi, naibu wangu James Nyoro na mwaasisi wa kampuni za Gakuyo na Ekeza David Kariuki Ngari,” amesema Waititu.

Amefafanua kuwa wanne hao ndio wamekuwa wakisambaza habari kila kona wakitumia majukwaa ya mawasiliano kuwa mtoto wake na mkewe ndio wanaiba mamilioni ya Kaunti ya Kiambu katika sakata ambayo Waititu anawajibishwa kujitetea na vitengo vya kupambana na ufisadi.

Waititu anadaiwa kuwa huenda ameiba jumla ya Sh588 milioni za kaunti ya Kiambu.

Akiongea katika afisi yake Kiambu na Taifa Leo kabla ya kufululiza hadi uwanja wa Ndumberi kuongoza sherehe za Madaraka Dei, amewataka wanne hao kupambana naye kisiasa kwa kuwa “binti yangu na mke wangu hawatasimama kuwania vyeo vya siasa 2022.”

Amesema kuwa hatari ya kuwaingiza watu wa familia yake katika mapambano ya kisiasa au ya ufisadi ni kuwa “unaweza ukawaelekeza majambazi kwao wakidhaniwa wako na pesa za kuibiwa.”

Amesema kuwa Wamatangi badala ya kuwa mratibu wa uthabiti wa Kaunti ya Kiambu amegeuka kuwa sauti ya utengano na vita vya kimaneno.

Hata hivyo, Wamatangi ameambia Taifa Leo kuwa Waititu mambo yanamwendea mrama

“Yeye ni kama nyani aliyetelezewa na miti na badala ya ashughulikie jinsi ataanguka bila madhara, anapiga kelele tu,” amesema Wamatangi.

Amesema kuwa kila pembe ambayo imesambaziwa pesa za wizi kutoka kwa kaunti lazima irejelewe katika vita vya kuokoa Kaunti hiyo.

Aidha, Waititu alisema kuwa vita kutoka kwa Kabogo vina kiini cha kijiba cha kushindwa 2017.

“Sasa ameamua kuwa vita vya kujirejesha katika mapenzi na wapigakura ni kunisingizia, kunikemea na kuchochea vita vya kisiasa katika kaunti,” amesema Waititu.

Naye Kabogo tayari amemwambia Waititu kuwa “masaibu uliyo nayo kwa sasa ni wewe umejiletea.”

“Unadhaniwa wizi na unafaa kujitetea kujinasua lakini sio kutapatapa kwa kila aliye karibu ukijaribu kumvuta kwa vita vyako vya kudhaniwa mfisadi,” akasema Kabogo.

Naye Nyoro amesemwa na Waititu kuwa amejiunga na vita dhidi yake kwa msingi kuwa “akionekana kunipiga zaidi ya wengine, akiwa naibu wangu basi ataibuka kuwa gavana 2022.”

Nyoro kwa upande wake ameteta vikali.

“Huyu gavana sio kiongozi bali ni tapeli ambaye alisaliti ndoto iliyotuweka pamoja kuibuka na ushindi 2017. Leo hii amegeuka kuwa dikteta wa kudhaniwa kila aina ya maovu na badala ya ajitetee kivyake, anasaka vijisababu kila mahali vya kufumba watu macho na masikio wasizingatie anachoulizwa hasa ambacho ni pesa za umma.”

Waititu amesema kuwa Kasisi Ngari amekuwa na mazoea ya kusema kuwa “mimi nilijipa pesa za wawekezaji wake wa Gakuyo na Ekeza.”

Gakuyo naye anasema kuwa Waititu ni dikteta asiyesemezeka na haambiliki ili ajipe kinga dhidi ya kuonekana akichovya asali ya Kaunti ya Kiambu.