Habari

Waititu akagua miradi ya maendeleo Wangige na Kikuyu

August 3rd, 2019 2 min read

Na SIMON CIURI na MARY WANGARI

IMEKUWA ni kazi kama kawaida kwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ambapo Jumamosi amekagua miradi kadha wakati kungalipo amri ya mahakama ya kumzuia kuingia afisini.

Bw Waititu aliyeachiliwa huru kutoka Gereza la Viwandani, Nairobi mnamo Alhamisi, Julai 31, aliendelea na majukumu yake kama bosi wa kaunti hiyo, ambapo alikagua miradi inayoendelea ya ujenzi wa Soko la Kikuyu pamoja na Hospitali ya Wangige ya Level Four inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Aidha, amedokeza kwamba ataongoza mkutano wa baraza lake la mawaziri mnamo Jumatano wiki ijayo, katika sehemu fulani atakayoichagua na wala sio katika afisi za kaunti, kwa mujibu wa ripoti.

Hatua ya Gavana huyu imejiri siku mbili tu baada ya kuachiliwa huru na kutozwa faini ya Sh15 milioni ambapo pia masharti ni kwamba haruhusiwi kuingia afisini mwake hadi kesi inayomkabili kuhusu sakata ya Sh588 milioni itakaposikizwa na uamuzi kutolewa.

Aidha, mwanasiasa huyo alitakiwa kuwasilisha nakala zake za usafiri mahakamani.

Akitoa uamuzi wake, Jaji wa Mahakama ya Kukabiliana na Ufisadi, Bw Lawrence Mugambi alisema kwamba “kuwazuia maafisa wa kaunti pamoja na kiongozi wao dhidi ya kuingia afisi zao kutawezesha kudumisha uadilifu wa kesi hiyo na pia kujali maslahi ya umma.”

Vilevile, mahakama ilitaja haja ya kuzuia aina yoyote ya kuingilia mashahidi kama sababu mojawapo ya uamuzi huo wa korti.

Uhalifu

Hatua hii ilijiri kufuatia uamuzi uliotolewa na Jaji Mumbi Ngugi kuhusu magavana wanaoshtakiwa dhidi ya visa vya uhalifu.

Katika uamuzi wake, Jaji Ngugi alihoji kwamba, magavana, sawa na watumishi wengine wa umma, wanafaa kukaa kando baada ya kushtakiwa kuhusiana na uhalifu na majukumu yao kuchukuliwa na manaibu wao.

Punde baada ya uamuzi huu, Naibu Gavana wa Kiambu, Bw James Nyoro ambaye pia ni hasimu mkuu wa Gavana Waititu kisiasa, aliandaa mkutano na vyombo vya habari ambapo alitangaza kuchukua usukani wa uongozi wa kaunti mara moja.

Uhasama umekuwa ukitokota kwa muda sasa kati ya Gavana Waititu na Naibu wake Bw Nyoro hivyo haikuwa ajabu alipotumia amri ya korti iliyomzuia mkubwa wake kuingia afisini, kujitwalia mamlaka kama kiongozi wa kaunti hiyo.