Habari Mseto

Waititu akosoa mahasimu wake kisiasa

May 11th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

GAVANA wa Kiambu amewataka wale wote waliomkashifu na kudai kuna ufisadi katika serikali yake wamwombe msamaha.

Bw Ferdinand Waititu alisema yeye Gavana wa Kiambu anatekeleza wajibu wake ipasavyo na yeyote aliye na ushahidi wowote kuwa aliiba fedha za  umma ana haki ya kuenda katika idara ya Polisi na kuandikisha taarifa huko.

“Watu wengi wamekuwa wakiniharibia jina kuwa eti mimi ni fisadi lakini hawana ushahidi wowote wa kunishtaki na kosa hilo. Sitatishwa na maongezi ya watu bali nitaendelea kuchapa kazi kama kawaida kwa sababu niliahidi wananchi kuwa nitakuwa mtumishi wao.

Baadhi ya wafanyakazi wakijiandaa katika uzinduzi wa barabara ya Juja Farm uliohudhuriwa na Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliyasema hayo Ijumaa alipozuru eneo la Juja Farm kunakojengwa barabara ya kisasa ya kilomita 12 kwa gharama ya Sh278 milioni.

Alisema barabara hiyo ikikamilika italeta maendeleo kwa wingi katika  eneo hilo.

Aliwahakikishia kuwa baada ya miezi mitatu hivi maji yatasambazwa kote Juja Farm na vitongoji vyake.

Alisema barabara hiyo kwa zaidi ya miaka 20 viongozi wamechaguliwa lakini hakuna lolote wameweza kutekeleza kuziweka katika hali nzuri.

“Ninamlaumu mtangulizi wangu Bw William Kabogo ambaye yaonekana ananionea kijicho kutokana na bidii yangu ya kutumikia wananchi. Tafadhali ningetaka aniachie nafasi nitekeleze wajibu wangu kwa amani,” alisema Bw Waititu.

Alimchamba naibu wake Bw James Nyoro kwa ‘kumkosea heshima’ na kumkashifu hadharani kutokana na maswala ya ufisadi.

“Kweli kama naibu wangu angekuwa mtu anayetaka maendeleo angekuwa amejua na kuelewa vyema yale yote yalikuwa yameorodheshwa katika maadishi ya bajeti jinsi ambavyo ilisomwa kwenye kamati ya fedha,”

Alisema naibu wake hutaka kudekezwa kwa kupangiwa kazi lakini ni sharti ajitume mwenyewe na kuzuru sehemu tofauti ili kuzindua miradi ya maendeleo.

“Lakini yaonekana jamaa huyu anataka nimdekeze kama mtoto ili afanye kazi. Mwanamume ni kujituma na kufanya kazi kikamilifu,” alisema Bw Waititu.

Alisema amejumuika na wananchi miaka mingi na anaelewa vyema ni kitu gani wanachokitaka.

Hata alisema amekulia katika mazingira ya uchochole, lakini mali yake amepata kutokana na bidii yake.

Alisema kuna miradi mingi inayohitaji kushughulikiwa haraka iwezekanavyo ambapo atafanya juhudi kuona ya kwamba inakamilika kwa miaka mitatu ijayo.