Habari

Waititu alia kuzimiwa simu na aliodhani ni marafiki

May 10th, 2020 2 min read

Na SIMONI CIURI

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu sasa anadai kuwa watu aliodhani kuwa marafiki zake na aliowasaidia kupata kura na wakashinda chaguzi wamemtenga na siku hizi hawajibu simu zake.

“Sasa nimeelewa siasa vizuri. Nilipokuwa Gavana wa Kiambu, nilikuwa nikipokea simu nyingi kutoka kwa wanasiasa waliotaka niwasaidie. Baadhi yao niliwasaidia kushinda chaguzi lakini sasa hawajibu simu zangu,” Bw Waititu alisema, bila kutaja majina.

“Sasa nami nimekoma kuwapigia simu kwani hiyo ndio hali ya siasa. Watu hukuhitaji tu wakati uko mamlakani na unaweza kuwasaidia sio baada ya kuondoka mamlakani,” Bw Waititu akalalama.

Gavana huyo wa zamani aliondolewa mamlakani na Bunge la Kaunti ya Kiambu mnamo Desemba 20, 2019 na hatua hiyo ikaidhinishwa na Seneti Januari 14, 2020.

Madiwani wa bunge hilo la Kiambu walimhusisha na sakata za ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake ya kutoa zabuni za mamilioni ya fedha kwa jamaa na marafiki zake.

Bw Waititu anasema kwamba sasa yeye ni raia wa kawaida baada ya kupokonywa magari ya serikali na walinzi.

Anasema kuwa mpaka sasa hajaelewa jinsi alivyoondolewa mamlakani kwa haraka jinsi hiyo.

“Rafiki yangu… Sasa mimi ni raia wa kawaida. Nilipokonywa magari ya serikali na walinzi wote dakika chache baada ya kuondolewa mamlakani. Sijui ni nani aliamuru kuwa magari hayo yaondolewe,” Bw Waititu akasema.

Aliongeza kwamba hata alirejesha mali za kaunti.

“Nilirejesha mali zote za kaunti. Sina chochote cha kaunti ya Kiambu ikiwemo baiskeli,” akaongeza.

Bw Waititu anasema wakati huu hataki kujihusisha na siasa lakini hiyo haimaanishi kuwa amestaafu kabisa kutoka siasa.

“Wanasiasa huwa hawastaafu. Nimechukua likizo ndogo tu, na nitarejea hivi karibuni,” akasema.

Gavana huyo wa zamani anasema wakati huu anajishughulisha na biashara zake za nyumba za kukodisha, mikahawa na magari ya uchukuzi wa abiria.

Bw Waititu anashikilia kuwa hataki kusema lolote kuhusu masuala ya serikali ya Kaunti ya Kiambu kwa sababu hahusiki katika uendeshaji wayo.

“Sitaki kuongea kuhusu Kaunti ya Kiambu. Kuna wale walioko mamlakani na wanaendesha shughuli za serikali jinsi wanavyotaka,” akasema Bw Waititu.