Waititu asema yuko ndani ya Kieleweke na Handisheki

Waititu asema yuko ndani ya Kieleweke na Handisheki

Na MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Ndung’u Waititu ametangaza Jumanne kwamba anaunga mkono juhudi za Rais Uhuru Kenyatta na washirika wake ndani ya mrengo wa Kieleweke na Handisheki.

Waititu ambaye pia hujulikana kama Baba Yao alihudumia Kiambu kati ya 2017 hadi Desemba 2019 ambapo alinga’atuliwa na Bunge la Kaunti ya Kiambu pamoja na Seneti Januari ya 2020 kisha akaandaliwa kesi kortini akidaiwa kupora zaidi ya Sh540 milioni.

Akiongea katika mji wa Juja ambapo anashiriki kampeni za Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Mei 18, Bw Waititu ambaye awali alikuwa mfuasi na mtetezi sugu wa Naibu Rais Dkt William Ruto ndani ya ‘Tangatanga’ ameelezea haja ya Mlima Kenya kuwa kitu kimoja.

“Kwa sasa ni vyema tujiunge pamoja kama Mlima Kenya nyuma ya Rais na tumtambue kama kinara wetu wa kijamii na kisiasa na hatimaye tumsaidie kupitisha BBI,” amesema Bw Waititu.

Kando na jinsi alivyokuwa akijipiga kifua kuwa hangemsaliti Dkt Ruto na alikuwa akiandamwa katika kesi ya ufisadi na kung’atuliwa kwa msingi wa imani hiyo yake ya kisiasa, Bw Waititu sasa amesema “tumtii Rais kama kiongozi wetu wa sasa na tumpe heshima anayohitaji kama kinara wa siasa zetu za Mlima Kenya.”

Bw Waititu amesema upo wakati ambapo busara ya mja humhitaji kuepuka vita na mirengo iliyo na nguvu na ni vyema “kumpisha mwenye nguvu.”

Awali alikuwa akipinga BBI na Handisheki lakini sasa anasema “BBI sio tu njema bali ni bora zaidi na Handisheki ni kitu cha maana kilicholeta utulivu na mazingara ya Rais wetu kuchapa kazi.”

Hivi majuzi, Seneta wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata aliteta kuwa “ukiwa unapinga Handisheki na BBI, unamulikwa na vitengo vya kupambana na ufisadi hapa nchini lakini ukitangaza unaunga mkono, hata ufisadi wako uwe unajiangazia bila kutafutwa, utaponyoka adhabu ya serikali.”

Bw Waititu amesema kwa sasa yeye ni mfuasi wa Rais na miradi yake ya kisiasa na kwamba yuko tayari kutii.

“Akielekeza nitakuwa mstari wa mbele kufuata maagizo,” amesema gavana huyo wa zamani.

Waititu amesema kuwa ratiba ya siasa za Rais kwa sasa ni kuwa “tufanye kazi kwanza, tupitishe BBI huku tukisukuma ajenda nyingine za kuleta maendeleo kama alivyoahidi akiomba kura za urais na hatimaye wakati wa kupanga siasa za 2022 ukifika, atatuita Ikulu ndogo ya Sagana na kutupa mwelekeo.”

You can share this post!

Vita vya serikali na usimamizi wa KTDA

Patson Daka: Fowadi matata wa Zambia anayenyima miamba wa...