Habari Mseto

Waititu awanasua mkewe, mwekezaji na vibarua mahakamani

August 16th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Kiambu Ferdinand Waititu aliwalipia dhamana wote walioshtakiwa, mkewe Susan Wangare Ndung’u, mwekezaji na vibarua 12 kwa kujenga jumba la orofa bila idhini ya kaunti ya Nairobi.

Bw Waititu aliwalipia jumla ya Sh1,140,000 ndipo waachiliwe.

Mkewe Gavana  huyo, muwekezaji Robert Okwaro na vibarua 12 walishtakiwa kwa kukaidi sheria za ujenzi.

Ikiwa mahakama itawapata na hatia kila mmoja atozwa faini ya Sh100,000 ama atumikie kifungo cha miaka miwili jela.

Bi Waititu alifikishwa katika Mahakama ya Citi saa nane mchana baada ya kutiwa nguvuni mwendo was aa nne asubuhi.

Alishikwa pamoja na mwekezaji aliyekuwa anaendelea na ujenzi wa orofa ya nane.

Bi Ndung’u alifikishwa mbele ya hakimu mkazi katika mahakama ya Citi Bi M W Njagi na kukana shtaka.

Alishtakiwa baada ya makabiliano makali kati ya Gavana Waititu na Gavana wa Nairobi Mike Sonko kwa njia ya simu.

Mazugumzo yao yalisambazwa katika mitandao ya kijamii ambapo Bw Waititu alisikika akiomba mkewe aonewe huruma na kuachiliwa.

Bw Waititu aliomba pia mjenzi na vibarua 12 waachiliwe pasi kushtakiwa lakini Bw Sonko akamweleza agizo la kumkamata mkewe limetoka “ juu”.

Bw Sonko alisikika akimweleza Bw Waititu mkewe awasilishe maombi ya kuidhinishiwa umiliki wa jumba hilo.

Wakili Manases Mwangi aliyemtetea Bi Ndung’u alifaulu kumtoa kwa dhamana ya Sh80,0000.

Kesi dhidi ya mkewe Waititu itatajwa mnamo Septemba 6, 2018 korti ielezwe ikiwa kiongozi wa mashtaka Bw Amos Gitahi amemkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi.