Habari Mseto

Waititu awapa tabasamu walioasi pombe hatari Kiambu

February 27th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KIAMBU ni mojawapo ya kaunti zinazotajwa kuathirika zaidi ambapo watu wengi ni walevi kupindukia.

Zaidi ya waliokuwa mateka wa ulevi 5,000 Jumanne walipokea hundi ya Sh20,000 kila mmoja ili kuwasaidia kujiimarisha kimaisha.

Gavana Ferdinand Waititu alisema hatua hii ni mojawapo ya ahadi zake kabla kuchaguliwa 2017, kutafutia vijana kazi.

Akizungumza katika hafla ya kufuzu kwa waathiriwa wapatao 5,200 uwanja wa Ndumberi chini ya mradi wa Kaa Sober, gavana hata hivyo alikashifu baadhi ya viongozi wanaomkosoa.

Alijitetea akieleza kwamba miradi ya maendeleo Kiambu haitafanyika ikiwa vijana wataendelea kusalia mateka wa pombe.

“Nilipokuwa nikiwaomba kura niliwaambia ‘Baba Yao’ hatawasahau. Tuliahidi vijana kazi, na ndio maana tunawapa pesa walioacha pombe. Wajiwekee kazi ili wajiimarishe,” akasema.

Viongozi wa Kiambu wanaomkosoa wanadai Waititu anatumia mradi wa Kaa Sober kufuja mamilioni ya pesa.

Tetesi ambazo hazijathibitishwa zinadai serikali ya kaunti hiyo hutumia pesa chungu nzima kila siku kuendesha mradi huo.

Alisema kufuatia juhudi zake katika vita dhidi ya pombe hasa haramu, visa vya wanaofariki kutokana na unywaji wake vimepungua. “Pombe iliyokuwepo awali imepungua. Hakuna siku nyingine Kiambu itakuwa na walevi kama ilivyokuwa kabla tuchaguliwe. Huu mradi tangu tuuanze, yale mazishi ya vijana tuliyokuwa tukihudhuria yamepungua kwa asilimia 90,” alieleza.

Alifichua kuwa kwa muda wa wiki mbili zijazo serikali ya kaunti ya Kiambu itazindua mfumo wa kutoa mikopo kwa vijana na kina mama, Jijenge Funds. Bw Waititu alihimiza waliofuzu kutumia mradi huo kuchukua mikopo ya kujiimarisha kuweka biashara.

Naibu gavana James Nyoro alitaja kufuzu kwa waasi hao kama mojawapo ya hatua kubwa, Kiambu imepiga mbele katika vita dhidi ya pombe. Kwa upande wake spika wa bunge la Kiambu Stephen Ndichu alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya maeneo yanayoendelea kugemwa na kuuzwa pombe haramu. “Kuna maeneo pombe haramu inapikwa na kuuzwa Kiambu, ninamuomba Bw Wanyama Musiambo aje tusaidiane kufanya oparesheni,” alisema. Musiambo ndiye naibu mkuu wa utumishi wa umma nchini, na amekuwa katika mstari wa mbele kupambana na bidhaa zisizoafikia ubora unaohitajika.

Kiongozi wa wengi bunge la Kiambu, Antony Ikonya alisisitiza kauli ya gavana Waititu kwamba miradi itafanyika endapo suala la pombe litadhibitiwa. Pia, alicharura wakosoaji wa Waititu akiwataka wajifikishe katika uwanja wa Ndumberi kushuhudia umati wa waliokuwa mateka wa pombe, walivyobadilika. “Hatutakubali barabara zipitiwe na walevi, na maji yanakosa wa kuyanywa. Tunataka asilimia 100 ya wakazi wa Kiambu wasiokunywa pombe,” alisema Ikonya, ambaye pia ni diwani, MCA wa Kiambu Mjini.

Peter Muhia, mwasi, ni mmoja wa walionufaika kupitia mradi wa Kaa Sober. Alisema alikuwa amenaswa na minyororo ya pombe haramu kwa muda mrefu, akizua ucheshi mama pima alipomkosa alitumana atafutwe. Alisimulia kuwa mke wake alimuachia mtoto wa miezi miwili kwa sababu ya kunywa pombe kupindukia na hata kumtwanga. “Nilishikwa mateka na pombe hata baada ya kuachwa na mke. Mtoto alipitia changamoto chungu nzima. Hata hivyo, mimi sasa ni kiumbe mpya,” alifafanua.

Madiwani ndio walikabidhiwa hundi ili kuwapa waasi. Kaa Sober ilianzishwa mwaka uliopita, 2018, ambapo waliojisajili walipokea mafunzo ya kozi mbalimbali za mikono na kiufundi kama useremala, ushonaji, uashi, mapishi na ususi, bila malipo katika taasisi za elimu ya juu 37 Kiambu kwa muda wa miezi mitatu. Wakiendelea kurekebisha tabia na maadili wamekuwa wakifanya kazi za kufagia barabara na kusafisha mitaro ya majitaka Kiambu, huku wakilipwa Sh400 kwa siku.

Mbunge mwakilishi wa wanawake Gathoni Wa Muchomba pia anaendesha mradi wa kunusuru waathiriwa wa pombe na dawa za kulevya Kiambu, ujulikanao kama Mamacare, ambapo yeye ni patroni wake. Bunge la kaunti hiyo mapema 2018, lilipitisha mswada wenye sheria za kusajili upya mabaa. Ofisi ya gavana ndiyo ilitwaa utoaji wa leseni kutoka mikononi mwa maafisa wa polisi, Waititu akisema hatua hiyo inalenga kudhibiti unywaji wa pombe.