Habari

Waititu kizimbani seneti mashtaka dhidi yake yakianza kusikizwa

January 28th, 2020 2 min read

Na PETER MBURU

GAVANA wa Kiambu Ferdinand Waititu, Jumanne amekuwa kizimbani Seneti kwa kusikizwa kwa mashtaka ya kutaka kumbandua, ambapo amejitetea kuwa makosa yake ni madogo, yasiyotosha kutimuliwa afisini.

Akionekana kutiwa moyo na hali kuwa magavana ambao hadi sasa wamefikishwa mbele ya Seneti kwa hoja za kuwaondoa walitakaswa na kurejeshwa kazini, Bw Waititu amesema ana imani kuwa pia naye atarejea Kiambu na kuendelea na kazi.

Bw Waititu pia ameonekana kuwatahadharisha maseneta wenye nia ya kuwania ugavana uchaguzi ujao kuwa chuma chao ki motoni, wasipompa haki.

“Nawasihi maseneta, kwa kuwa najua wengi wenu mtakuwa magavana mnamo 2022, mkumbuke mtakuwa hapa kizimbani kama mimi na mtahitaji kutendewa haki. Pia mimi nilikuwa upande mliopo wakati mmoja na sasa niko kizimbani,” Gavana huyo ameambia Seneti.

Aidha, Bw Waititu ambaye alizuiwa kukanyaga afisini na korti zaidi ya miezi miwili iliyopita kutokana na kesi anayokumbana nayo ya ufisadi, amelaumu ‘vita vya propaganda’ kuwa ndivyo vimemletea shida hizo.

Amelaumu Bunge la Kaunti ya Kiambu kuwa lilikosa kumsikiza kabla ya kufikia uamuzi wa kumtimua, na kuwa pia lilivunja sheria, kwani madiwani waliokuwapo bungeni siku hiyo hawakutosha kupitisha hoja ya kumbandua.

Gavana huyo anawakilishwa na mawakili Ng’ang’a Mbugua, Peter Wanyama na Charles Njenga, nalo Bunge la Kaunti linawakilishwa na mawakili Naani Mungai na Karuga Maina, na madiwani Solomon Kinuthia (Ndenderu), Gideon Gachara (Ndeiya) na Yvonne Wanjiku.

Anakumbwa na mashtaka ya ukosefu wa uadilifu katika usimamizi wa rasilimali za kaunti, kwa kulimbikizia kaunti madeni ya hadi Sh4 bilioni, kudharau Bunge la Kaunti na kulemaza shughuli zake, matumizi mabaya ya ofisi na kupanga kupora shamba la mjane mjini Thika.

Wawakilishi wa bunge la Kiambu waliambia Seneti wana ushahidi wa kutosha kuhusu madai hayo, wakiitaka imbandue.

“Haogopi hata kichapo cha mwenyezi Mungu,” akasema wakili aliyezungumza kwa niaba ya Bunge la Kaunti.

Spika wa Seneti Ken Lusaka amesema Bw Waititu atapewa fursa ya kusikizwa na Seneti Jumatano, kisha maseneta watashiriki kikao cha faragha kujadiliana kuhusu suala lenyewe, kabla ya kupiga kura.

“Seneti inatambua uzito wa suala hili na itahakikisha kuwa linasikizwa kwa haki,” Bw Lusaka akasema.