Wajackoyah atikisa wagombea wakuu

Wajackoyah atikisa wagombea wakuu

NA CHARLES WASONGA

MGOMBEAJI urais wa chama cha Roots Party of Kenya, George Wajackoyah amezua msisimko wa aina yake katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 kwa kuibua masuala tata miongoni mwa Wakenya.

Prof Wajackoyah, ambaye anapambana na William Ruto wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Raila Odinga wa Azimio la Umoja Kenya One na Mwaure Waihiga wa Agano Party amezua mvuto mkubwa hasa miongoni mwa vijana ambao wanamtazama kama anayezungumza lugha yao ya mageuzi na uhuru wa maamuzi.

Kabla ya kuidhinishwa kuwa mwaniaji, Prof Wajackoyah hakuchukuliwa kwa uzito na wawaniaji wakuu ambao ni Dkt Ruto na Bw Odinga, lakini sasa wameanza kumwangazia hasa baada ya ahadi zake kuanza kuzua mijadala pamoja na kuvutia sehemu ya Wakenya ambao wanamwona kama tofauti na wawili hao ambao wamekuwa kwenye siasa kwa miaka na mikaka.

Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot ameonya kwamba huenda Prof Wajackoyah akalazimisha awamu ya pili ya uchaguzi wa urais: “Ikiwa Wajackoyah atafanya kampeni kali na kufaulu kupata angaa kura 500,000, anaweza kuzuia Dkt Ruto ama Bw Odinga kupata ushindi katika awamu ya kwanza. Anatoa ahadi za kiajabu ambazo zinavutia vijana na watu wa tabaka la kadri.”

UMAARUFU

Kwenye kura ya maoni iliyotolewa wiki hii na kampuni ya Trends and Insights for Africa (Tifa) katika Kaunti ya Nairobi, Prof Wajackoyah alipata umaarufu wa asilimia saba licha ya kuanza kampeni zake wiki chache tu zilizopita, ikilinganishwa na Dkt Ruto na Bw Odinga ambao wamekuwa wakijipigia debe tangu 2018.

Mnamo Jumatano, Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee chake Rais Uhuru Kenyatta, David Murathe alikiri wanamfuatilia kwa makini Prof Wajackoyah na kauli zake, na kuwa wanatilia maanani baadhi ya mapendekezo yake kama vile kuhalalishwa kwa ukuzaji bangi kwa ajili ya kuuzwa ng’ambo.

“Tumemshauri mgombea urais wa muungano wetu, Raila Odinga kuhalalisha ukuzaji wa bangi kwa sababu za kibiashara. Kiwango cha faida ambacho Wajackoyah anataja hakifai kupuuzwa,” Bw Murathe akasema jana asubuhi kwenye mahojiano katika runinga ya NTV.

Kisheria bangi ni marufuku nchini na adhabu kwa anayepatikana akiitumia ama kuuza ni kali sana.

Prof Wajackoyah amekuwa akisisitiza kuwa nia yake sio bangi kutumiwa na Wakenya kama dawa ya kulevya, bali ni ya kuuza nje ya nchi kwa ajili ya kutumika kutengeza dawa ya matibabu.

Kulingana na Profesa Wajackoyah, ambaye pia ni wakili, gunia moja – la bangi – la uzani wa kilo 50 linauzwa kwa Sh386 milioni katika masoko ya Amerika.

“Ikiwa Kenya itauza magunia 50 inaweza kulipa madeni yake baada ya mwaka mmoja au miaka miwili. Kero ya ufisadi pia itapungua kwa sababu wananchi watakuwa na pesa mfukoni,” Prof Wajackoyah akasema Jumatatu kwenye mahojiano katika kituo cha Spice FM.

KUKASHIFIWA

Kwa upande mwingine Prof Wajackoyah na mgombeaji mwenza wake Justina Wambui Wamae wamekashifiwa vikali hasa na viongozi wa kidini, wazazi na watu wengine wenye misimamo mikali ya masuala ya maadili na jamii.

“Viongozi wa kidini wanaonipiga vita hawajaelewa manifesto yangu. Aina ya bangi ambayo tutahalalisha ni ile inayotumika kutengeneza dawa wala sio ile ya kulewesha, na ambayo imevuruga maisha ya watu, haswa vijana wetu,” Profesa Wajackoyah akaeleza.

Pia amekanusha kutumia bangi: “Sivuti bangi, sigara na sinywi pombe. Lakini nitavuta mara moja nikiingia Ikulu ili kutakasa nchi.”

Mnamo Jumapili wiki jana, muungano wa Maskofu wa Kanisa Katoliki (KCCB) uliwaonya Wakenya dhidi ya kumpigia kura mgombea huyo wa urais wakisema sera zake zinalenga kuvuruga maisha ya vijana.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nyeri, Antony Muheria, ambaye aliongea kwa niaba ya wenzake, alisema mpango huo wa Profesa Wajackoyah pia utarudisha nyuma kasi ya maendeleo nchini.

“Tunawataka wapiga kuwa kuwakataa wanasiasa ambao wanapanga kuharibu maisha ya vijana wetu kupitia uhalalishaji wa bangi. Bangi, sawa na dawa zingine za kulevya, ni sumu katika mipango ya maendeleo ya nchi na ndio maana imepigwa marufuku kulingana na sheria za Kenya,” akaeleza Askofu Muheria.

Kando na kuhalalisha bangi, Profesa Wajackoyah pia ameahidi kustawishaji ufugaji nyoka kwa ajili ya kuvuna sumu ya kutengenza dawa za matibabu.

Pia ameahidi kuanzisha hukumu ya kifo kwa washukiwa wa ufisadi kama njia ya kumaliza uovu huo nchini, haswa serikalini: “Nitafanya hivyo, kwa kusimamisha utekelezaji wa kipengele cha katiba kinachosema kuwa mshukiwa hana hatia hadi rufaa zote kuhusu kesi yake zisikizwe na kuamuliwa.”

  • Tags

You can share this post!

Bunduki 22, risasi 500 zapatikana katika nyumba mtaani...

Safari ya mgombeaji urais wa Roots kutoka Uganda hadi alipo...

T L