Habari Mseto

Wajakazi waandamana wakitaka watambuliwe kama sekta rasmi

February 22nd, 2018 1 min read

Na LUCY KILALO

WAFANYAKAZI wa Nyumbani Jumatano waliandamana wakitaka kutambuliwa kama sekta rasmi humu nchini na kuthaminiwa.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Nyumbani, Hoteli, Taasisi za Elimu na Hospitali (KUDHEIHA), Bw Albert Njeru, walisema kuwa wajakazi wa nyumbani hawaheshimiwi, na baadhi ya watu wanawalipa kwa kuwatupia nguo kuu kuu.

“Wakati umefika tutambuliwe, tulipwe mshahara kama mfanyakazi yeyote mwingine, wakati umefika tupewe likizo ya siku 21 kama wafanyakazi wengine, tutambuliwe kama wafanyakazi, tupate bima ya matibabu (NHIF), Malipo ya Uzeeni (NSSF), tunataka kulindwa na sheria ya Kenya na pia kimataifa.

Mfanyakazi wa nyumbani lazima awe kama wale wengine wako kwa ofisi,” alisema Bw Njeru.

Wafanyakazi wa nyumbani waandamana nje ya majengo ya Bunge la Kitaifa jijini Nairobi Februari 21, 2018 wakitaka watambuliwe kama wafanyakazi wa ofisini. Picha/ Lucy Kilalo

Wafanyakazi hao katika Barua yao kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Jumatano walisema kuwa wanataka kuona Mkataba wa Shirika la Leba la Kimataifa (ILO) Nambari 189 kuhusiana na kazi yenye heshima kwa wafanyakazi wa nyumbani ikiratibiwa humu nchini.

Mbunge wa Emuhaya, Omboko Milemba, ambaye ni katibu wa chama cha Kuppet, na mbunge Maalum Godfrey Osotsi, walipokea barua hiyo kwa wafanyakazi hao waliokuwa wameandamana nje ya majengo ya bunge.

Bw Milemba alisema kuwa watahakikisha bunge linapitisha mkataba huo akitaja wafanyakazi hao muhimu kwa jamii.