Pambo

Wajakazi wafananisha kuosha nguo za ndani za mabosi na ‘uchawi mamboleo’

January 14th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

BAADHI ya wajakazi jijini Nairobi wametoa malalamishi kwamba mabosi wao huwafanyia ‘uchawi mamboleo’ kwa kuwapa mavazi ya ndani kuosha.

Wengi wakiwa ni weusi, wanahisi kwamba mavazi ya ndani yanafaa kuwa siri ya anayevaa, kumaanisha ndiye anayestahili kuosha.

Wanasema hawana tatizo kuosha mavazi ya aina hiyo na ambayo ni ya watoto wa mabosi wao.

Wajakazi hao hupokea mishahara tofauti kutegemea na eneo ambalo anafanyia kazi. Katika mitaa inayofahamika kuwa ni ya wadosi kama vile Karen, Kileleshwa na Lavington, wengi wa wajakazi hao walisema hulipwa Sh15,000 kila mwezi na wale ambao hufahamika kuwa mama fua, hulipwa Sh1,500 mara moja kwa wiki.

Mitaa iliyosalia, wajakazi wengi waliambia safu hii kwamba hulipwa chini ya Sh10,000 kwa mwezi na mama fua hupokea Sh500 kwa kila rundo la nguo.

Mjakazi mmoja kutoka mtaa wa Kibra, *Anita anayefanya kazi ya nyumba katika mtaa wa Lang’ata, alisema mwajiri wake wa asili ya Kihindi humlipa Sh9,000 kila mwezi.

*Anita alisema alijipata katika njia panda siku ya pili hapo kazini alipolazimika kufanya usafi wa nyumbani ambao unajumuisha kufua nguo. Alikumbana na vijivazi vya ndani vya mwajiri wake huyo alizohitajika kuziosha.

“Niliambiwa niende maliwatoni kuchukua nguo zote zilizokuwa humo ambapo nilikutana na nguo hizo za ndani za mama, baba, watoto wa kiume na wa kike. Kila siku wanapooga, wanaziacha nguo hizo kwa bafu zikiwa chafu,” akasema *Anita.

Alisema hulazimika kufanya kazi hiyo ilimuradi kupata pesa na kuepuka uzushi wa mara kwa mara na bosi wake.

“Unapata zile nguo ni chafu kupindukia. Lakini pia nimewahi kulazimika kuokota mipira ya kondomu zilizotumika na kutupwa kwenye sakafu. Kila siku nalazimika kuomba Mungu anipe kazi nyingine. Wakati mwingine nalia lakini nikikumbuka mahitaji ninayo, ninajipa nguvu,” akasimulia.

Mjakazi mwingine, *Mariana, anasema yeye ni mhafidhina anayeegemea kwa utamaduni wa kabila lake ambapo ni mwiko kuosha mavazi hayo.

Yeye anasema kuwa licha ya kuajiriwa, analazimika kuacha mavazi hayo kwenye kikapu cha nguo.

“Tamaduni zetu ni tofauti duniani ila kuna watu ambao hawajali wengine. Si dhambi kumwelewa mwenzako,” akasema *Mariana.

Akaongeza: “Wakinipatia chupi zao ziwe safi au chafu, sitafua. Haswa ukiwa mwenye afya, utazipata nimerudisha kwenye kapu la nguo ujioshee mwenyewe.”

Bi Jacklyne Kavochi ambaye amefanya kazi hiyo ya ujakazi nchini Saudi Arabia kwa miaka tisa, kupitia njia ya simu, alisema kila bosi ana tabia zake na akawataka wajakazi kuelewa waajiri wao na ikiwezekana, wakae chini wazungumzie suala hilo.

Ijapokuwa anatumia mashine kufua nguo za ndani, anasema baadhi ya waajiri hutaka pia zipigwe pasi.

“Wajakazi wasishangae wakiulizwa na mzee wa nyumba iliko nguo yake ya ndani,” akasema Bi Kavochi.

Alidai kuwa baadhi ya wake wa waajiri wao, mara nyingi wanakuwa tu kwa simu wakifurahia uhondo kwa Tiktok wajakazi wakiulizwa alisema Bi Kavochi.

Nchini Italia, raia hawaoni tatizo ambapo wanawake huosha nguo za ndani za watoto wao waliotinga umri wa miaka 18.

Utafiti wa shirika la Oxfam Kenya unaonyesha kuwa wajakazi wengi hutoka katika mitaa ya Kibera, Mathare, Mukuru, Kawangware na Korogocho jijini Nairobi. Utafiti huo ulionyesha kuwa wanawake na wasichana hutumia saa 11 kwa siku kufanya kazi hiyo.