Habari Mseto

Wajane mjini Ruiru wapewa chakula

June 25th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAJANE wanastahili kulindwa ili kuepushiwa balaa na dhuluma wanazopitia.

Naibu Gavana wa Kaunti ya Kiambu Bi Joyce Ngugi alisema Jumanne wajane wanastahili kulindwa ili wasidhulumiwe baada ya kupoteza waume zao.

Alisema serikali ya kaunti itaendelea kuwajali baadhi yao kwa kuwapa kazi na zabuni wakati wowote fursa zikipatikana kwa kuzingatia sheria na uadilifu.

“Kwa muda mrefu wajane wamepitia masaibu mengi ya kifamilia na kwa hivyo ni vyema kuwajali popote walipo,” alisema Bi Ngugi.

Aliyasema hayo mjini Ruiru alipowakabidhi chakula zaidi ya wajane 50 waliofika ili kupokea msaada huo.

“Sisi viongozi katika Kaunti ya Kiambu tutawasilisha mswada katika bunge la kaunti ili kutenga fedha za kuwasaidia wajane ili wajikimu kimaisha,” alisema Bi Ngugi.

Mjane Bi Dayanah Kamande alisema wajane wengi wamepitia masaibu mengi katika jamii.

“Wengi wa wajane hulaumiwa kuwa ndio wamewaua waume zao, jambo ambalo linasababisha kutengwa zaidi na jamaa zao,” alisema Bi Kamande.

Alisema umefika wakati ambapo wajane wanastahili kuja pamoja ili kutetea haki zao popote walipo.

“Wajane wanastahili kuunda kikundi cha kuwa pamoja ili kuwa na sauti moja hasa katika kulinda maslahi yao. Iwapo tutafuata hivyo, bila shaka tutapata nguvu kama kitu kimoja,” alisema Bi Kamande.

Alisema wanawake wengi hupata shida kulinda mali zilizoachwa na waume zao au walizozalisha kwa pamoja na waume kabla mauti.

“Jambo hilo limekuwa likiendelea kwa muda mrefu na kwa hivyo, umefika wakati wajane waje pamoja na kutetea haki zao,” alisema Bi Kamande.