Wajawazito 550 hufa kila mwaka wakijifungua Kilifi – Ripoti

Wajawazito 550 hufa kila mwaka wakijifungua Kilifi – Ripoti

NA ALEX KALAMA

LICHA ya juhudi za serikali kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha akina mama wanajifungua hospitalini salama bado idadi ya mama wanaoaga dunia wakati wa kuzaa ingali juu kaunti ya Kilifi.

Kulingana na mshirikishi wa afya ya uzazi kaunti ya Kilfi Kenneth Miriti ni kwamba vifo vya akina mama wanaofariki wakati wa kuzaa vimefikia 551 kwa mwaka kati ya akina mama laki moja wanaojifungua kila mwaka kaunti hiyo.

Akizungumza na wanahabari katika zahanati ya Mnarani wakati wa kupeana mafunzo ya uzazi kwa akina mama Miriti, alisema hatua hiyo inatokana na akina mama wengi kujifungua nyumbani huku wengine wao wakiaga baada ya kujaribu kuavya mimba.

“Visa vya kina mama kufa katika hospitali sio vingi kama ambavyo nimeelezea wanawake ni kama wanawake 80 kwa laki moja ambao wanakufa kule hospitalini,” alisema Bw Miriti.

Hata hivyo afisa huyo wa afya alidokeza kuwa kulingana na deta ya serikali akina mama 551 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na mimba wanazobeba.

Kitengo cha watoto wachanga katika Hospitali ya Kilifi. PICHA | ALEX KALAMA

Kwa upande wake Shallet Anzazi ambaye ni muuguzi katika zahanati hiyo ya Mnarani alisema kuwa kufikia sasa wamerekodi akina mama wengi kuhudhuria kliniki na hata kuzalia hospitalini hali ambayo imepunguza kwa asilimia kubwa ya vifo vya akina mama waja wazito.

“Na watu ambao wanakuja kupata hizi huduma za kliniki ni wengi halafu pia kwa sababu tunawapatia ile kadi ya linda mama. Vifo vya wakina mama vimepungua si kama pale zamani mama alikuwa kwa sababu anataka kujifungua na hana uwezo atang’ang’ana kule nyumbani mpaka mwishowe tumpoteze. Lakini saa hii anajua niko na linda mama kwa hiyo hata kama mimi nitaenda kushindwa kuzaa. Kwa sababu ya matatizo nikifanyiwa upasuaji linda mama inanisaidia kufanyiwa upasuaji na sitalipa chochote,” alisema Bi Anzazi.

Naye Zeinab Thuva ambaye amefanya kazi ya kuhamasisha jamii kwa maswala ya afya yani Community Health Volunteer kwa zaidi ya miaka kumi sasa amewashauri akina mama kuhudhuria kiliniki wanapobeba mimba ili kupunguza vifo vya akina mama.

“Waje wazalie hospitalini kwa sababu kuzalia nyumbani kuna hatari,pengine yule mtoto ni mkubwa nafsi ya mama ni ndogo. Umezaa mimba mbili tatu lakini yule ni mkubwa pengine ni kilo nne ni kilo tano nafsi yake ni ndogo akizaa nyumbani anapasuka. Kuna ule ugonjwa wa kukojoa ovyo ovyo unaturudia sisi inatubidi tumuchukue tena tumpeleke hospitali kwa sababu amepasuka njia yote mbele na nyuma. Kwa hivyo tuna wahimiza wazazi waeze kuzaa hospitalini kwa sababu wakizaa huko kwanza atajulikana njia yake iko sawa. Pili akionekana ana matatizo gani na tatu atasaidiwa uzazi wake azae mtoto mzuri, ” alisema Bi Thuva.

  • Tags

You can share this post!

Mvua ya unga yanyeshea raia

Familia za waliokufa kwenye mauaji ya Wagalla zataka fidia

T L