Habari Mseto

WAJIR: Gavana ataja wafugaji wa kuhamahama kama sababu ya kuongezeka kwa visa vya Covid-19

May 18th, 2020 2 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

GAVANA wa Kaunti ya Wajir Mohammed Abdi amewataja wafugaji ambao wanaingia na kutoka ndani ya kaunti hiyo kama sababu ya kuongezeka kwa idadi ya visa vya ugonjwa wa Covid-19 katika eneo hilo.

Kaunti ya Wajir ni ya tatu nchini iliyorekedi visa vingi zaidi vya maambukizi baada ya Nairobi na Mombasa.

Visa vilivyorekodiwa ni vya wafugaji wanaoingia nchini kutoka Somalia.

Kwa sasa Wajir imerekodi visa 15 vya watu waliyoambukizwa Covid-19 ambapo 14 ni wale walioingia Wajir kutoka Somalia.

Alisema hali hiyo inatokana na mipaka kutokuwa na ulinzi wa kutosha kudhibiti matembezi ya watu.

“Tumeweka maafisa wa kutosha ili kuhakikisha kuwa wanaoingia wanapimwa kabla ya kuruhusiwa kujumuika na watu wengine,” akasema.

Kulingana na Waziri wa Afya katika kaunti hiyo, Bw Ismail Issack alisema japo hawajaandikisha vifo kutokana na ugonjwa huo, idadi ya maambukizi inaogofya.

Aidha maafisa wa afya walisema kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa huo na mila zimechangia wakazi kukiuka masharti yaliyowekwa na wizara ya afya ili kudhibiti ugonjwa huo.

“Watu hawazingatii sheria ya kutokaribiana. Wengine wanatembea katika sehemu za umma bila kuvaa vitamvua, watu bado wanasalimiana kwa mikono bila kujali kuwa wanahatarisha hali zao za afya,” akasema afisa wa afya Bw Said Omar.

Hamasisho

Licha ya serikali kufanya hamasisho kupitia vituo vya redio, wengi wa wakazi bado wanalalamikia kutokuwa na ufahamu wa kutosha wa jinsi ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo hatari.

“Uhamasisho unafanywa kupitia vyombo vya habari, lakini kuna watu ambao hawana redio. Wanaotuweka katika hatari ya maambukizi ni wafugaji ambao wengi wao hawana muda wa kusikiliza matangazo kutokana na mila yao ya kutokaa sehemu moja,” akasema mkazi wa jina Bi Hafsa Mustafa.

Mkazi mwingine, Hassan Feisal alisema kuwa wakati huu ukiwa mwezi wa Ramadhan wakazi wanashiriki ibada na hawana muda wa kusikiliza matangazo kutoka kwa redio.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa soko kuu katika eneo hilo linaendeleza shughula za kawaida, huku asilimia 50 pekee ya wauzaji wakifuata masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya.

Kiwango cha juu cha maambukizi katika kaunti hiyo kilisababisha Rais Uhuru Kenyatta kufunga mpaka wa Kenya na Somalia kama njia ya kudhibiti maambukizi.