Wanasiasa wajiuza kwa jina la Mungu

Wanasiasa wajiuza kwa jina la Mungu

MWANGI MUIRURI NA BENSON MATHEKA

WAWANIAJI wakuu wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 wamegeukia kutumia jina la Mungu kujiuza kwa wapigakura.

Wanasiasa hao hasa William Ruto wa muungano wa Kenya Kwanza na Raila Odinga wa Azimio la Umoja wakati huu wa kampeni ‘wamekumbatia’ dini kiasi cha kuweza kuamua ni nani aliye na imani kuliko mwingine.

Dkt Ruto amekuwa kwenye mstari wa mbele kujiuza kwa jina la Mungu na kumdunisha Bw Odinga kama mwenye ‘imani za uganga’.

Bw Odinga, ambaye amekuwa akijifananisha na Joshua katika Biblia aliyevukisha wana wa Israeli Mto Jordan hadi Canaan, amekuwa akijitetea dhidi ya madai hayo.

“Mimi ni muumini wa kanisa la Angilikana la Kenya,” Bw Odinga alijitetea majuzi.

Dkt Ruto pia amefahamika kwa kunukuu aya za Biblia mara kwa mara katika hafla mbalimbali katika juhudi za kuonyesha yeye ni mcha Mungu.

Naibu Rais pia ana sifa ya kutoa michango minono makanisani akisema anatimiza hitaji la kutoa sadaka kulingana na Ukristo, lakini wakosoaji wake wamemlaumu wakisema anaitumia fursa hiyo kutafuta ushawishi kutoka kwa waumini.

Dkt Ruto na Bw Odinga katika kipindi hiki pia wamekuwa wakijitokeza kuonyesha imani yao hasa wanapovalishwa mavazi ya kidini na kupiga magoti kuombewa na wahubiri.

Katika mikutano ya ibada, wanasiasa hawa wamekuwa wakihakikisha hotuba na picha zao wakiwa makanisani zinafikia wafuasi wao kote nchini kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Pia wamekuwa weledi wa kutumia salamu za kidini za jamii tofauti kuchangamsha wanaohudhuria mikutano yao ya kampeni.

Jumapili iliyopita, Dkt Ruto aliongoza washirika wake kuhudhuria ibada katika kanisa la Jesus Winner Ministry Roysambu, Nairobi ambako alinukuu Biblia. Hii ilikuwa siku chache baada ya kukutana na ujumbe wa wahubiri kutoka Kibra, Nairobi katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi.

Mnamo Jumapili, Bw Odinga na mgombea mwenza wake katika muungano wa Azimio, Martha Karua walihudhuria kongamano la kila mwaka la dhehebu la Akorino nchini lililofanyika katika uwanja wa michezo wa Kasarani. Japo lilikuwa kongamano la kidini, hotuba za viongozi zilihusu uchaguzi mkuu.

Kulingana na mtaalau wa masuala ya kidini Dkt Pricilla Kandie, wanasiasa hutumia makanisa kufikia wapigakura msimu wa kampeni za uchaguzi.

“Huu ni mtindo unaotumiwa na wanasiasa msimu wa kampeni za uchaguzi ingawa kwenye uchaguzi wa mwaka huu umevuma sana kwa sababu ya ushindani na kila mgombeaji kutaka kuonekana kuwa mcha Mungu kwa sababu suala la maadili limepatiwa kipaumbele,” asema Dkt Kandie.

Kwenye kampeni za mwaka huu, wanasiasa wamekuwa wakihudhuria mikutano ya madhehebu mbalimbali wanakotoa hotuba wakijifanya wanyenyekevu.

Tofauti na kabla ya msimu wa kampeni za uchaguzi, Wakenya hawakuwa wakiona wanasiasa makanisani kwa makundi na hata wale waliokuwa wakihudhuria ibada hawakuwa wakitangaza katika mitandao ya kijamii ilivyo kwa wakati huu.

Mnamo Mei 29, mwaniaji mwenza wa Bw Odinga, Martha Karua alihudhuria kongamano la wanawake wa kanisa la Presbyterian Church of East Africa (PCEA) lililoandaliwa Thogoto Kiambu, aliposifu kanisa kwa mchango wake wa siasa na utulivu nchini. Kabla ya kuteuliwa mgombea mwenza hakuwa akichangamkia mikutano kama hiyo.

“Tunachoshuhudia kwa wakati huu ni mbinu ya kujivumisha msimu huu wa uchaguzi ili waonekane wanaheshimu Mungu. Wanatumia ibada kujipendekeza kwa wapigakura kwa sababu huwa hawagharimiki isipokuwa sadaka wanayotoa,” asema Dkt Kandie.

Kwa upande wake, mwaniaji urais wa chama cha Roots, George Wajackoya amesisitiza yeye ni kuhani wa dini ya Kihindi ya Krishna na kuwa anatekeleza ibada zake kikamilifu.

  • Tags

You can share this post!

Eliud Kipchoge na INEOS waanzisha kituo Kaptagat kukuza...

Mwaniaji urais apoteza kesi na kuomba chupa ya maji

T L