Wajomvu sasa wataka warudishiwe ardhi yao

Wajomvu sasa wataka warudishiwe ardhi yao

Na WACHIRA MWANGI

JAMII ya Wajomvu katika Kaunti ya Mombasa, inataka uchunguzi kuanzishwa kuhusu dhuluma za kijadi dhidi yao, ili kuiwezesha kurudishwa katika ardhi yake ya ekari 150 katika eneo la Jomvu Kuu.

Kwenye barua ya iliyowasilisha kwa Kamati ya Seneti kuhusu Ardhi, jamii iliirai kamati kuharakisha mchakato wa kutatua mzozo kuhusu umiliki wa ardhi hiyo yenye nambari ya usajili 162/V/M.N. CR1070.

Jamii hiyo huwa inaishi katika wadi ya Jomvu Kuu Village, Kata Ndogo ya Jomvu.Jamii hiyo ni miongoni mwa jamii 12 za asili ya Uswahilini zilizoanza kukaa Mombasa karibu miaka 800 iliyopita, kulingana na barua hiyo.

Ilidai kuwa mnamo 1846, mmishenari Dkt Ludwig Krapf kutoka Ujerumani alifika Pwani ya Afrika Mashariki na kukaa eneo la Rabai, ambako alijenga kanisa lake. Kamati iliambiwa jamii imekuwa ikitumia ardhi hiyo kwa shughuli kama kilimo na kufikia maeneo ya kuvulia samaki kwa muda mrefu.

Vile vile, imekuwa ikitumia sehemu yake kama makazi.Hata hivyo, mzozo ulizuka baada ya Kanisa la Methodist kuanza kuigawanya na kuuza baadhi ya vipande vyake kwa watu kutoka maeneo mengine.Jamii ilisema kuwa kwa muda huo wote, imekuwa ikishikilia ardhi hiyo kama makao yake asili.

Ilisema haina mahali pengine inakoweza kwenda kutafuta makao.Bw Akseli Lameck, ambaye ni mkazi, aliiomba Seneti kusimamisha uuzaji huo, akiutaja kuwa kinyume cha sheria na njama ya kuwanyang’anya wenyeji umiliki.

Jamii pia ilieleza hofu kuwa huenda njia za kuelekea eneo la Jomvu Maunguja, ambalo huwa inatumia kuingia baharini kuvua samaki ikafungwa.

Ilisema maeneo mengine yatakayoathiriwa makaburi ya mababu zao, maeneo ya kidini na kitamaduni, hali ambayo itairejesha nyuma sana.Hata hivyo, Tume ya Kitaifa kuhusu Ardhi (NLC) iliahidi kuchunguza suala hilo.

“Tumepokea ombi lenu. Tuko hapa kumsikiliza na kutoa mapendekezo ambayo yatamsaidia kumrejeshea umiliki wa ardhi yenu. Kama NLC, tunafahamu kwa undani suala hili na tumeamua kushirikiana ili kutafuta suluhisho la kudumu,” akasema mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Gershom Otachi.

Kamati hiyo pia iliahidi kuchunguza madai kuwa polisi waliwapiga na kuwahangaisha wenyeji. Iliwarai polisi kuwalinda wenyeji na mali yao badala ya kuwatesa.

Wenyeji waliwalaumu polisi kwa kuwapendelea baadhi ya mabwanyenye huku wakiwahangaisha.Hata hivyo, kamati iliahidi kufikisha ujumbe huo kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai.

You can share this post!

Ghasia katika kampeni za UDA

Shule za bweni zipigwe marufuku – Kuppet