Habari MsetoSiasa

Wajukuu wasema Moi alitenga muda kuwa nao

February 12th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

FAMILIA, jamaa marafiki, wanasiasa na viongozi mbalimbali jana waliungana kutoa wosia na heshima zao katika siku ya mwisho ya kumpumzisha aliyekuwa rais wa pili nchini Kenya Daniel Toroitich Arap Moi, katika ibada ya mazishi iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Kabarak, Nakuru.

Watoto, wajukuu, vitukuu pamoja na marafiki wa karibu wa rais huyo mstaafu walikuwa na kumbukumbu za kuyeyusha nyoyo kumhusu Mzee Moi zilizodhihirisha picha tofauti kabisa ya marehemu na kumsawiri kama baba mwenye mapenzi na aliyetenga muda kila mara kukaa na watoto wake.

Baadhi waliwavunja mbavu waombolezaji huku wakisimulia nyakati maalum walizoshiriki na Mzee Moi aliyefariki mnamo Februari 4 kabla ya mazishi yake nyumbani kwake Kabarak.

Wajukuu wasichana wa Mzee Moi wakiongozwa na Laila Cherobon walimsomea shairi babu yao lenye anwani ‘Safari ya Mwisho.’

“Jambo la mwisho ninalokumbuka nilipokuwa na babu yangu pamoja na binti yangu ambaye ni kitukuu wa babu yangu ni kwamba ‘Cherobon, kila wakati kumbuka kumweka Mungu mbele na usichukulie kirahisi kila kitu ulicho nacho. Kwa sababu kila kitu nilicho nacho na vyote utakavyokuwa navyo ni kwa neema ya Mungu,”

“Pia nakumbuka kila mara babu alikuwa akisema kamwe usiweke imani yako kwa binadamu kwa sababu mwanadamu kila wakati atakuvunja moyo lakini kila mara weka imani yako kwa Mungu,” alisema Bi Cherobon

Mjukuu wa kwanza wa Mzee Moi ambaye ni mwanawe marehemu Jonathan Moi, Bw Clint Kiprono, alimwomboleza babu yake akisema kwamba likizo katika familia yao hazitakuwa za kawaida tena kufuatia kifo cha Mzee Moi.

“Alikuwa mtu wa hadhi kuu mno kiasi kwamba wakati mmoja jina Moi lilikuwa sawa na kusema rais. Nilipokuwa mdogo, utani uliokuwepo ulikuwa ‘Moi wa Uganda ni nani? Kwa sisi wajukuu wake alitufunza umuhimu wa kuwa na maono, unyenyekevu na zaidi upendo wa Yesu ambaye ndiye nguzo ya hekima yote,”alisema Bw Kiprono.

Bw Kiprono alisimulia jinsi babu yake alivyojawa na furaha wajukuu na vitukuu wake walipozaliwa na alivyofurahia kukaa nao.

“Nitakosa mambo mengi sana kuhusu babu yangu. Ushauri wake, maneno ya kuhimiza na kuwatia moyo wajukuu wake na imani yake katika uwezo wetu. Lakini zaidi nitakosa kukaa naye tukitazama vipindi vya wanyama na habari. Likizo kwa familia ya Moi hazitakuwa sawa tena. Furaha iliyoonekana machoni mwake alipowaona wajukuu na vitukuu vyake haina kifani,”

Marafiki wa karibu wa Mzee Moi wakiwemo daktari wake binafsi Dkt Silverstain alimwomboleza Mzee Moi akimtaja kama rafiki na kukumbuka jinsi alivyopenda kula nyama na divai kidogo kutoka Israeli aliyoiita ‘dawa ya wazee’ waliyoshiriki pamoja na Bw Charles Njonjo.

“Nilikutana kwa mara ya kwanza na Mzee mnamo 1972 akiwa naibu rais mwenye umri wa miaka 60 nami nikiwa daktari wa moyo mwenye umri wa miaka 33 na tukaanza uhusiano wetu wa miaka 42,”

“Mzee alikuwa mgonjwa mzuri aliyefuata maagizo lakini kuna jambo moja tu nililoshindwa kumshawishi kuacha. Kufanya kazi kupita kiasi. Nililazimika hata kunukuu kifungu kwenye Kitabu cha Kutoka Jethro alipokuwa akimshauri Musa,” alisimulia.