Kimataifa

Wajumbe mbioni kuhakikisha Trump na Kim Jong-Un wamekutana

May 29th, 2018 2 min read

Na AFP

WASHINGTON, AMERIKA

WAJUMBE wa Amerika na Korea Kaskazini wamekutana kurejelea uwezekano wa kuandaliwa upya kwa kikao kati ya Rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong- un.

Kwenye mazungumzo hayo, yaliyofanyika mnamo wikendi, ilidhihirika kwamba Rais Trump ameelezea nia ya kukutana na Kim, licha ya mkutano huo kufutiliwa mbali katika hali tatanishi.

Kwenye jumbe kadhaa alizoandika katika akaunti yake ya Twitter, Bw Trump aliisifia Kaskazini, akiitaja kuwa ni nchi iliyo na uwezo mkubwa kiuchumi. Bw Trump pia alisema kuwa “hatajali kushauriana” na Kim nafasi nyingine itokeapo.

“Naamini kwamba Korea Kaskazini ina uwezo mkubwa sana kiuchumi, ambapo itakuwa nchi ya kupigiwa mfano siku moja,” akasema Bw Trump. Akaongeza: “Kim anakubaliana nawe kuhusu hili. Itatimia!” akasema.

Aidha, alithibitisha kwamba kundi la wajumbe wa Amerika wamefika Kaskazini kufanya maandalizi ya kikao hicho.

Msimamo huo wa Trump unatofautiana na kauli yake siku kadhaa zilizopita, ambapo alifutilia mbali mkutano kati yao wawili.

Akieleza sababu ya hatua hilo, Bw Trump alisema kuwa alichukua hatua hiyo kutokana na “msimamo mkali wa Kaskazini kuhusu mpango wake wa urutubishaji wa zana za kinuklia.”

Lakini siku kadhaa baada ya kauli hiyo, Amerika ilianza harakati za kidiplomasia kuondoa dhana hiyo, kwa msingi kwamba “bado kuna nafasi ya mashauriano.”
Mikakati hiyo ililenga kufufua maandalizi mapya ya mkutano huo.

Mnamo Jumamosi, Bw Kim alikutana na Rais Mo Jae-in wa Korea Kusini, katika mpaka wa nchi hizo mbili, ili kuangazia mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati yake na Amerika.

Kulingana na maandalizi mapya, kikao hicho kimepangiwa kufanyika mnamo Juni 12 nchini Singapore.

Mipango hiyo pia imethibitishwa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Amerika, kwa kusema kuwa maandalizi ya kikao hicho yanaendelea.

“Tuko katika hatua za mwisho mwisho za maandalizi ya mkutano huo muhimu,” akaeleza msemaji wa wizara hiyo Bi Heather Nauert.

Gazeti la ‘The Washington Post’ liliripoti kwamba ujumbe wa Amerika uliofika Kaskazini uliongozwa na balozi wa zamani wa Amerika katika Korea Kusini na Kaskazini Susan Kim.

Gazeti pia liliripoti kwamba ujumbe huo ulikutana na Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kaskazini Choe Son Hui.

Kwa sasa, Amerika haina balozi katika Kusini, licha ya juhudi zinazoendelea za kurejesha uhusiano wake wa kidiplomasia.

Kulingana na wachanganuzi, cha muhimu kwa sasa ni kungoja matokeo ya mkutano kati ya viongozi hao wawili.