Habari Mseto

Wakazi Nairobi kuzidi kukosa maji

December 17th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAKAZI wa Nairobi wataendelea kukabiliwa na uhaba wa maji bidhaa hiyo ikisambazwa kwa vipimo hata ingawa mabwawa ya Ndakaini na Sasumua yamefurika kufuatia mvua kubwa inayoshuhudiwa katika nyanda za juu za Aberdares.

Kwenye taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jumanne kampuni ya Maji na Maji Taka ya Jiji la Nairobi (NCWSC) ilisema kuwa hali hiyo imechangiwa mabomba (pipes) yake kutoweza kupitisha kiwango hitajika cha maji.

Kampuni hiyo ilisema wakati huu mabomba yake yana uwezo wa kusafirisha lita 525,600 ya maji kwa siku moja, kiwango ambacho ni chini ya kiwango cha maji ambacho kinahitajika kukimu mahitaji ya wakazi wa Nairobi kwa siku.

“Usambazaji wa maji kwa vipimo utaendelea hadi pale tutakapojenga mabomba mapya makubwa ya maji. Wakati huu hitaji la maji ni lita 790,000 kwa siku na hitaji hilo linapanda kuwa lita 20,000 kila mwaka kutokana na ongezeko la watu jijini,” taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa NCWSC Bw Nahashon Muguna.

Mabomba ya sasa ya maji yalinuiwa kuhudumia jiji la Nairobi hadi mwaka wa 2000 lakini serikali imechelea kupanua miundo mbinu hiyo ili kutimiza kupanda kwa hitaji la maji.

Wakati huu wakazi wa Nairobi katika mitaa mbalimbali hukabiliwa na uhaba wa maji huku mitaa inayoathirika zaidi kuwa Lang’ata, Umoja na Kawangware.

Hali hii ya uhaba wa maji imepelekea baadhi ya wakazi kutegemea maji inayosambazwa na watu waliounganisha paipu kinyume cha sheria, vioski vya kuuza maji na wachuuzi ambao wengi wao wanauza maji ambayo usafi wake ni wa kutiliwa shaka.

Baada ya wachuuzi wa maji katika mitaa mbalimbali huuza bidhaa hiyo kwa kati ya Sh20 na Sh100 kwa mtungi mmoja wa lita 20.

Kampuni ya NCWSC ilianza kusambaza maji kwa mgao mnamo mwaka wa 2o17 kutokana na kupungua kwa maji kiwango cha maji katika bwawa la Ndakaini ambako asilimia 80 ya maji inayotumika Nairobi hutoka.

Lakini hali hiyo, ya usambazaji maji kwa vipimo, imeendelea kushuhudiwa hata wakati huu ambapo bwawa hilo limejaa kupita kiasi kufuatia mvua kubwa ambayo inaendelea kunyesha.

Chini ya mpango wa sasa wa usambazaji maji kwa vipimo, wakazi wa jiji hupata maji kwa siku chache ndani ya wiki huku wengine hukaa hata kwa wiki kadha bila bidhaa hiyo muhimu.

Mnamo Julai 2017 kulitokea mkurupuko wa kolera iliyosababisha vifo vya watu watatu. Lakini serikali ya akaunti ya Nairobi ilielekeza kidole cha lawama kwa wachuuzi wa maji iliyodai wamekuwa wakiuza maji yasiyo safi.

Serikali ya kaunti ya Nairobi sasa inategemea kukamilishwa kwa mradi wa ujenzi wa bomba kubwa lenye urefu wa kilomita 11.8 maarufu kama Northern Water Collector Tunnel ili kuiweza kuimarisha usambazaji wa maji jijini.

Ujengo wa bomba hilo umepangiwa kukamilika mnamo Desemba mwaka kesho wa 2020.

Bomba hilo litakusanya maji kutoka mito ya Maragua, Gikige na Irati katika kaunti ya Murang’a na kuyaelekeza katika bwawa la Ndakaini. Hata hivyo, hatua hii haitasuluhisha kero la maji jijini hadi mabomba ya maji ya kampuni ya NCWSC zitapanuliwa.