Habari Mseto

Wakana mashtaka 151 ya kughushi hati za ajali kudai fidia

August 24th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAAJENTI wawili feki Ijumaa walifunguliwa mashtaka 151 yaliyochukua muda wa saa moja unusu kusomwa na hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi.

Ilibidi Bw Andayi asaidiwe na karani wa mahakama kuwasomea mashtaka hayo Mabw Nicholas Koech na Kennedy Odada Kadema.

“Mashtaka dhidi yenu ni mia moja na hamsini na moja. Haya ndiyo mashtaka mengi zaidi kuwahiwasilishwa mbele yangu tangu nianze kufanyakazi ya Uhakimu. Lakini kwa vile yamewasilishwa na upande wa mashtaka unaoongozwa na Bi Kajuju Kirimi sina budi ila kuwasomea kila shtaka,” Bw Andayi aliwaeleza washtakiwa.

Aliongeza , “Baada ya kuwasomea kila shtaka kila mmoja wenu atajibu shtaka. Ama akubali ama akatae. Je mngelipenda kutumia lugha ipi mahakamani? Kuna lugha ya Kiswahili ama lugha ya Kiingereza,” Bw Andayi aliwaeleza.

“Tungelipenda utusomee mashtaka kwa lugha ya Kiswahili,” washtakiwa walimjibu.

Watu waliokuwa wamefika kortini kufuata kesi za watu wa familia zao walipigwa na butwaa na kushangaa kusikia wawili hao walikuwa  wanakabiliwa na mashtaka 151.

Mmoja wa watu alisikika na Taifa Leo akiuliza , “Naona watasomewa mashtaka haya mpaka kesho.”

Hakimu hakumjibu ila aliwataka washtakiwa wawe makini ndipo waelewe mashtaka dhidi yao.

“Nataka muwe makini. Sikizeni kila shtaka na kujibu kwa ufahamu,” Bw Andayi alishauri.

Hakimu pia aliwaeleza mukhutasari wa kesi dhidi yao akisema , “Mashtaka yote 151 yanahusu ughushi wa stakabadhi za ajali ambayo  ilitokea katika eneo la kaunti ya Kajiado.

Mnadaiwa mlijitengenezea stakabadhi mbali mbali ambazo mlimpelekea wakili Janet Wekesa katika jengo la  Rehema House na kumweleza hati mlizompelekea zilikuwa halisi.”

Bw Andayi alianza kuwasomea washtakiwa mashtaka dhidi yao.

Shtaka la kwanza lilisema walighushi stakabadhi waliyodai imesajiliwa na Afisa Mkuu wa Polisi ya Kajiado.

Stakabadhi hiyo walisema ilikuwa imepewa Bi Elizabeth Muoki wakidai alikuwa amehusika katika ajali ya barabara iliyotokea katika barabara ya Kajiado Namanga.

Mbali na stakabadhi hiyo ya polisi , pia washtakiwa walishtakiwa kwa kosa la kughusi hati za matibabu wakidai zimetoka katika Hospitali ya Serikali ya  Kajiado .

Washtakiwa hao walikabiliwa na shtaka lingine la kughushi hati za Picha za X-Ray za Elizabeth wakidai ni halisi zilizotayarishwa na hospitali hiyo ya Kajiado.

Washukiwa hao walishtakiwa kuwa walimpelekea wakili Bi Janet Wekesa wakidai zilikuwa hati halisi za mlalamishi Bi Elizabeth Muoki aliyehusika katilka ajali ya  barabara.

Mabw Koech na Kadema walikabiliwa na mashtaka mengine yakughushi hati za Bw Peter Wanjala, Bi Emily Muchangi , Bw Mulwa Kimolo, Bi Janet Nduku na Bw Justus Aroko miongoni mwa wengine.

Pia walighushi hati za matibabu kutoka hospitali za Kinoo Medical kaunti ya Kiambu na Shalom Hospital iliyoko katika kaunti ya Machakos.

Washtakiwa walighushi hati za matibabu wakidai zimetiwa saini na Dkt E K Mwaura na zilikuwa halali.

Mahakama iliwaachilia washtakiwa kwa dhamana ya Sh500,000 kila mmoja na kutenga Septemba  26, 2018 kuwa siku ya kusikizwa.