HabariSiasa

Wakati ukitimia njoo Pumwani ujifungue bila malipo, Sonko aambia Waiguru

July 14th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

HATA kabla ya saa 24 kukamilika baada ya Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kufunga ndoa na wakili Kamotho Waiganjo, Gavana wa Nairobi Mike Sonko amemtaka Bi Waiganjo kutafuta huduma za kujifungua wakati utakapofika katika hospitali ya Pumwani bila malipo.

Bw Sonko, ambaye anafahamika kwa kutoa matamshi ya kutatanisha Jumapili asubuhi alimkaribisha Bi Waiguru katika hospitali hiyo, akisema huduma zimeboreshwa kuwa za kiwango cha juu.

Gavana Sonko aliendelea kusema kuwa mkewe anatarajiwa kujifungulia katika hospitali hiyo miezi kadhaa ijayo.

“Nampongeza Gavana Anne Waiguru kwa kuolewa na wakili Waiganjo kwa niaba ya familia yangu na wakazi wa Kaunti ya Nairobi. Nakutakia kuwa na kujifungua kwema wakati utakapofika.

Unakaribishwa katika hospitali ya Pumwani ambapo mke wangu pia anatarajiwa kujifungua miezi kadha ijayo,” Bw Sonko Jumapili akaandika katika akaunti yake ya Facebook.

Ni maneno ambayo alitumia wakati amekuwa akiendeleza juhudi za kuboresha utoaji huduma wa hospitali hiyo, baada ya kukumbwa na sakata si haba, kuhusu wizi wa watoto na idadi kubwa ya watoto waliokuwa wakifariki wakati wa kina mama kujifungua, kwa miaka mingi.