Habari MsetoSiasa

Wakati wa kuvunja serikali umefika, viongozi Rift Valley wamwambia Uhuru

March 3rd, 2019 2 min read

Na TITUS OMINDE

BAADHI ya wabunge na wafuasi wa chama cha Jubilee wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta avunje serikali iwapo anaamini kuwa ufisadi umekita mizizi serikalini.

Mbunge wa Kimilili Bw Didmus Barasa alisema iwapo Rais anaamini kuwa kuna ufisadi serikalini kama inavyodaiwa hana budi kuvunja serikali ili Wakenya wachague viongozi wapya.

Bw Barasa alisema wale wanaodai kuna ufisadi serikalini ni watu ambao wanampiga vita naibu rais ili asigombee urais 2022.

Bw Barasa alilaumu kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga ambaye alidai anatumia muafaka kati yake na Rais kumpiga vita Naibu Rais William Ruto.

Akihutubu katika eneobunge la Kapseret wakati wa harambee ya kuchangisha pesa za kusaidia ujenzi wa kanisa la AIC Kimoson ambapo aliandamana na mbunge wa eneo hilo Bw Oscar Sudi, Bw Barasa alisema siasa za handisheki zinatumiwa kumdunisha Naibu Rais wala si kuunganisha Wakenya.

Bw Barasa alionekana kutofautiana na viongozi ambao wanadai kuna ufisadi serikalini huku akimtaka Rais kupuuza watu kama hao na kuangazia ajenda ya Jubilee ya maendeleo kwa Wakenya

“Iwapo Rais anaamini kuna ufisadi serikalini hana budi kuvunja serikali yote na kuitisha uchaguzi upya ili kuondoa viongozi ambao wanashukiwa kuwa wafisadi,” alisema Bw Barasa

Bw Barasa alisema uongozi wa Jubilee haufurahii hatua ya rais kutoa nafasi kwa kiongozi wa ODM kuingilia masuala ya uongozi serikalini hasa sera za Jubilee.

Msimamo wake uliungwa mkono na mbunge wa Kapseret Bw Sudi ambaye alimtaka Rais Kenyatta kutangaza hadharani iwapo anataka Katiba ifanyiwe marekebisho ili apate kipindi kikingine cha kuwania urais na kukiuka mkataba kati yake na Naibu wake William Ruto.

Kuhusu vita dhidi ya ufisadi, Bw Sudi alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma George Kinoti anatumiwa na maadui wa Bw Ruto.

Naye gavana wa kaunti ya Uasin Gishu Bw Jackson Mandago alidai vita dhidi ya ufisadi nchini vimatumiwa kisiasa huku akikosoa namna suala la ufisadi katika mabwawa linavyoendeshwa.

Bw Mandago alidai kuwa kuna watu serikalini ambao hawafurahii azma ya Ruto ambao wameingiza unafiki katika vita hivyo kwa lengo la kudunisha Naibu wa Rais.