Kimataifa

Wakatoliki wataka ufafanuzi kuhusu Papa kuunga ushoga

October 24th, 2020 2 min read

KAMPALA, Uganda

Na MASHIRIKA

KANISA Katoliki nchini hapa linataka ufafanuzi kuhusu ripoti kwamba Kiongozi wake Duniani, Papa Francis ameunga ndoa ya watu wa jinsia moja huku suala hilo likiibua hisia mseto miongoni mwa waumini ulimwenguni.

Msemaji wa Muungano wa Maskofu wa Kanisa hilo Uganda, Kasisi Philip Odii alisema ufafanuzi kutoka makao makuu ya Kanisa yaliyoko Vatican City, utaliwezesha kutoa mwongozo kwa waumini wake nchini Uganda.

Katibu Mkuu wa Muungano huo John Baptist Laura amemwandikia barua mwakilishi wa Papa nchini Uganda Askofu Mkuu Luigiu Bianco akiitisha taarifa rasmi kutoka afisi ya Papa Francis kuhusu suala hilo.

Kasisi Odii aliwaambia wanahabari kwamba kanisa hilo nchini Uganda haliwezi kutoa msimamo wowote kuhusu suala hilo kabla ya kupokea taarifa rasmi kutoka Roma.

“Hili ni suala ambalo hatujalielewa; tunahitaji kujua kile hasa Papa alisema kwa sababu kwa kawaida, makao makuu ya Kanisa Katoliko hutoa taarifa kufafanua kauli anazotoa Papa,” Kasisi Odii akawaambia wanahabari Ijumaa.

Habari zimetanda katika vyombo vya habari vya kimataifa zikiashiria kuwa Papa Francis aliunga mkono ndoa kati ya watu wa jinsia moja.

Kulingana na shirika la habari la CNN, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alitoa kauli hiyo katika filamu kwa jina “Francesco” iliyoelekezwa na mtengenezaji filamu Evgeny Afineevsky, ambaye ni raia wa Urusi. Filamu hiyo ilionyeshwa jijini Roma Jumatano katika tamasha ya maonyesho ya filamu.

“Mabasha wana haki ya kuoana na kuanzisha familia. Wao ni watoto wa Mungu. Hakuna mtu anayepasa kutengwa na kudharauliwa kuhusu suala hilo,” Papa Francis anaripotiwa kusema katika filamu hiyo.

Aliongeza kuwa; “Kile tunahitaji ni kuunda sheria ya mahususi ya kulinda ndoa kati ya watu wa jinsia moja. Sheria kama hiyo itahalalisha ndoa kama hizo.”

Katika mahojiano ya awali, Papa Francis amewahi kudokeza kuwa hapingi ndoa za kiraia; lakini hii ndiyo mara ya kwanza kwake kujitokeza wazi kuunga mkono ndoa za watu wa jinsia moja.

Kauli yake kuhusu suala hili nyeti inakinzani na ya mtangulizi wake, Papa Benedict XVI, ambaye alichukulia ndoa aina hizo kama zisizokubalikana kwani zinaenda kinyume na hali ya maumbile. Kimsingi, aliharamisha ndoa kati ya mabasha na wasagaji.

Katika miaka ya nyuma, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kianglikana nchini Uganda yamekashifu ndoa za jinsia moja yakisema zinaenda kinyume na mafundisha ya Bibilia Takatifu.