Habari Mseto

Wakazi 500 wa Nyali wanufaika na bima ya afya kutoka mfuko wa NG-CDF

August 29th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

WATU 500 kutoka eneobunge la Nyali mjini Mombasa wamefaidika na bima ya afya iliyofadhiliwa na mfuko wa hazina ya NG-CDF eneo la Nyali.

Wengi waliopata ufadhili huo ni wazee na walemavu.

Watu hao walikabidhiwa kadi zao Ijumaa katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Kongowea katika hafla iliyohudhuriwa na Naibu Rais William Ruto, mbunge wa Nyali Mohammed Ali, mwakilishi wa eneo la Kongowea Abrari Mohammed, wa Freere Town Charles Kitula, aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar miongoni mwa viongozi wengine.

Alisema ufadhili huo utawasaidia wasiojiweza kupata matibabu bora.

Naibu Rais William Ruto aliongezea nusu milioni akiomba watu zaidi waongezwe kwa mradi huo.

“Kwa maendeleo ya nchi ni lazima wanachi waweze kupata matibabu bora na usalama. kutakuwa ma mfuko ambao tumeweka milioni mbili kuwawezesha mayatima na wazee kupata mapato kila mwezi,” akasema Dkt Ruto.

Aidha alizindua maktaba katika eneo la Kongowea ambapo alisema itasaidia wakazi wa Nyali.

“Watoto wekuwa wakitembea hadi Mombasa mjini kusoma; hii itawapunguzia mwendo. Pia nitawafadhili na vipakatalishi 50 kuwezesha wanafunzi kufanya utafiti na kusoma mitandaoni,” akasema.

Alisema maktaba hiyo ni ya kuboresha elimu katika eneo hilo.