Habari Mseto

Wakazi Juja wataka watumiwe wanajeshi kukabiliana na fisi

January 7th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI 

WAKAZI wa Juja sasa wanaitaka serikali itume kikosi cha jeshi (KDF) eneo hilo ili kukabiliana na genge la fisi ambalo limekuwa likiwahangaisha na hata kusababisha maafa.

Kwa mujibu wa mshirikishi wa masilahi ya wakazi wa Juja Bw Simon Wambugu, fisi hao wameua zaidi ya watu 20 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Alhamisi, Januari 4, 2024, iliyopita wakiua kijana wa miaka 10.

“Lakini kwa sasa baada ya fisi hao kuua watu watano katika kipindi cha mwezi mmoja katika maeneo ya Nyacaba, Juja Farm na viunga vya maeneo hayo, serikali imetuma maafisa wa Shirika la Wanyamapori nchini (KWS) kushirikisha msako unaofahamika kama Operation Ondoa Fisi,” akasema Francis Wambugu, mkazi.

Bw Wambugu alisema kwamba maafisa hao sasa wamemaliza mwezi mmoja na wamefanikiwa kunasa fisi 12 “huku ikikadiriwa kwamba kuna zaidi ya fisi 1, 000”.

Alisema kwa sasa “kero hili linafaa kupewa kikosi cha jeshi wa nchi kavu ili wakabiliane na fisi hao kama majangili wa uvamizi wa mauaji na kwa kuwa tunajua maafisa hao huwa kwa kawaida hawataki kujiangazia kama wa kufeli, afueni tutaipata chini ya siku 10”.

Alisema maafisa hao wakiingia na vifaru na bunduki zao kubwakubwa pamoja na mabomu, hao fisi watatimiziwa ajenda ya maangamizi.

Tayari, Gavana wa Kiambu Bw Kimani wa Matangi ameteta kwamba KWS imeonyesha mapenzi sana kwa wanyama hao badala ya kuwajibikia usalama wa binadamu.

“Ningetaka kutoa onyo kwa KWS kwamba watwambie kati ya maisha ya fisi na binadamu ni gani ya thamani. Mimi sitaongea kuhusu suala hili tena. Nitatuma matingatinga kufukua mashimo ambayo wanyama hao hujificha na nifyeke vichaka vyote hadi wafe wote,” akasema.

Hata hivyo, KWS kupitia taarifa rasmi mnamo Desemba 31, 2023 ilisema kwamba vita dhidi ya fisi hao vinaendelezwa ipasavyo kwa mujibu wa malengo.

Huduma hiyo kwa wanyama ilisema kwamba “nia yetu sio kuua fisi hao kinyume na sheria lakini ni kuwashughulikia kwa mujibu wa mikakati iliyowekwa”.

Aidha, KWS iliwakosoa wenyeji kwa kuchukulia vita hivyo kama kiini cha sinema ya kujiburudisha.

“Unapata raia usiku wa giza wakiwa wanatufuata vichakani kushuhudia vile tunapigana na fisi hao. Raia wanasema wanataka kuona tukitumia bunduki na risasi ili wajipige ‘selfie’ nasi pamoja na fisi hao,” akasema afisa mmoja.

Aliteta kwamba “tukiwaamrisha waondoke, wanajificha kwenye vichaka vilivyo karibu kiasi cha kutukanganya tukiwadhania ni fisi, hali ambayo ni hatari sana hata kwa maisha yao ikizingatiwa ni eneo la operesheni ambalo hata risasi zinatumika”.

 

[email protected]