Wakazi Lamu wakataa kafyu kurefushwa

Wakazi Lamu wakataa kafyu kurefushwa

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa sehemu za Kaunti ya Lamu wanaishinikiza serikali isiongeze muda wa kafyu walioekewa baada ya mashambulio yaliyotokea Januari.

Mnamo Januari 5, 2022, Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i aliorodhesha maeneo zaidi ya 10 ya Lamu kuwa sehemu zinazotatizika kiusalama, hivyo kuweka kafyu ya siku 30.

Hii ni baada ya shambulio lililosababisha vifo vya watu 15, na zaidi ya nyumba 10 kuteketezwa.

Wakiongozwa na Diwani wa Wadi ya Hongwe, Bw James Komu, wakazi hao walisema wanashindwa kujitafutia riziki kwani wanalazimika kurudi majumbani mwao mapema.

“Tunahisi kafyu inakandamiza uhuru wetu wa kujitafutia. Ifikapo saa kumi na moja unusu au saa kumi na mbili jioni, maafisa wa usalama wanakutarajia uwe umemaliza shughuli za siku. Kuna wamiliki wa biashara ambazo zinafanya vyema zaidi nyakati za usiku. Hata sisi viongozi pia uhuru wetu wa kusafiri hakuna,” akasema Bw Komu.

Juhudi za kumpata Kamishna wa Lamu, Bw Irungu Macharia, ili aeleze kuhusu uwezekano wa kafyu kuondolewa hazikufua dafu kwani simu hakujibu simu alipopigiwa.

Bw Joseph Mwangi ambaye ni mhudumu wa bodaboda mjini Hindi alikiri kuwa familia nyingi eneo hilo zinakumbwa na njaa kwani shughuli nyingi za kiuchumi.

Aliiomba serikali kuja na mbinu mbadala, ambapo doria za walinda usalama ziongezwe lakini kuwe na uhuru wa kujitafutia majira yote.

Bi Lucy Maina ambaye ni mmiliki wa duka mjini Kibaoni alisisitiza haja ya serikali kudumisha ushirikiano na wananchi ili wawe huru kuwapasha habari wakati wowote wanaposhuhudia matukio ya kigaidi maeneo yao.

Alikashifu tabia ya baadhi ya maafisa wa usalama na jeshi ambao wamekuwa wakitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia.

“Hata wakaweka hii kafyu muda wote, ikiwa ushirikiano baina ya raia na walinda usalama hautadumishwa, sidhani hivi visa vya utovu wa usalama vitamalizwa. Kafyu iondolewe, doria za walinda usalama ziongezwena ushirikiano wa jamii na walinda usalama idumishwe,” akasema Bi Maina.

You can share this post!

Saudia yawekeza kwa mradi wa matini ya dijitali kujinyanyua...

Wakulima walia hasara kwa kukosa soko la matunda

T L