Wakazi Malindi wafurika barabarani kusherehekea Aisha Jumwa kuteuliwa waziri

Wakazi Malindi wafurika barabarani kusherehekea Aisha Jumwa kuteuliwa waziri

NA ALEX KALAMA

WAFUASI wa aliyekuwa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa wamesherekea baada ya Rais William Ruto kumteua awe Waziri wa Maswala ya Utumishi wa Umma alipotaja Baraza la Mawaziri jana Jumanne.

Wakiongozwa na Bendera Charo, wakazi hao wamempongeza Rais Ruto kwa kutambua juhudi za wanawake wakisema hatua hiyo imeonyesha wazi kwamba yeye ni kiongozi asiyekuwa na ubaguzi.

Akizungumza na wanahabari mjini Malindi, Charo amesema Ruto ndiye rais wa kwanza ambaye ameweza kupatia nafasi ya uwaziri mwanamke kutoka jamii ya Wagiriama katika eneo la Pwani.

“Tunamshukuru rais kwa kuweza kutambua juhudi za mama Aisha Jumwa. Hii imetutia moyo sana sisi wanawake wa Kilifi kwa sababu ametuonyesha wazi kwamba anatujali na anatutambua. Na sisi tunaahidi kusimama na yeye wakati wote na tunamuombea Mwenyezi Mungu azidi kumpa afya njema na hekima ili aongoze Wakenya vizuri,” alisema Charo.

Hata hivyo, Charo amewataka viongozi wote wa Kilifi ambao wamechaguliwa kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kushirikiana ili kuhudumia wananchi kwa njia ya usawa pasipo kuwabagua kwa misingi ya kisiasa, dini wala kabila.

“Pia nataka kutuma salama kwa wale wote waliochaguliwa hapa Kilifi kwamba wakati wa siasa umeisha, sasa kilichobakia ni kufanyia wananchi kazi. Kwa hivyo mkaweze kuinamisha vichwa vyenu pamoja na muangalie jinsi ambavyo mtaweza kushughulikia yale matatizo ambayo yanawakumba wakazi wa Kilifi ikiwemo njaa,” alisema.

Wafuasi wa aliyekuwa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa wakisherehekea baada ya Rais William Ruto kumteua awe Waziri wa Maswala ya Utumishi wa Umma alipotaja Baraza la Mawaziri mnamo Septemba 27, 2022. PICHA | ALEX KALAMA

Naye aliyekuwa mgombea kiti cha Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kilifi kupitia chama cha UDA Juliet Riziki Baya amempongeza Aisha Jumwa kwa kuteuliwa kuwa waziri akisema alikuwa anastahili kutunukiwa nafasi hiyo kutokana na mchango wake wa kujitolea kuvumisha UDA.

“Mimi nataka kumshukuru Rais kwa kumtunuku dada yetu Aisha nafasi ya uwaziri, hii imedhihirisha wazi kwamba Ruto ni rais wa kusema na kutenda. Safari ya UDA hapa Kilifi ilianzishwa na Aisha Jumwa nasi tunasema Asante Ruto kwa kumkumbuka Aisha. Umetupatia nguvu sisi akina mama wa Kilifi, akina mama wa¬† Kigiriama… Hivi sasa naye msichana wa Kilifi atasoma akimuangalia Aisha Jumwa pale juu. Mwenyezi Mungu akubariki na akupe nguvu uongoze Kenya kwa amani,” alisema Bi Baya.

Naye aliyekuwa mwaniaji wa kiti cha ubunge wa Malindi kupitia chama cha UDA Daniel Chiriba amempongeza Ruto kwa kupatia eneo la Pwani nyadhifa kubwa za uongozi katika serikali yake.

“Imeonekana wazi kwamba katika historia Ruto wewe ndiye rais wa kwanza kutambua eneo la Pwani kwa kutupatia mawaziri wawili pamoja na spika wa bunge la seneti. Na hii ni kuonyesha unatupenda na unatutambua sisi watu wa Pwani. Pili nataka kukushukuru kwa kurudisha huduma za bandari katika jiji la Mombasa na hii itasaidia vijana wengi wa Pwani kupata ajira. Na sisi kama watu wa Pwani tunahisi kuinuliwa sana na serikali yako,” alisema Bw Chiriba.

  • Tags

You can share this post!

MCAs kutumia Sh10 milioni katika warsha Mombasa

ZARAA: Wajukuu wanafurahia matunda ya bidii yake

T L