Habari

Wakazi Mombasa bado wasubiri miradi hewa ya Gavana Joho

February 1st, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

WAKAZI wa Mombasa wanaendelea kusubiri ahadi za Gavana Hassan Joho kuhusu miradi mikuu ambayo ilipaswa kukamilika 2019.

Bw Joho alipoapishwa kuhudumu kwa muhula wa pili, aliahidi angetekeleza mradi wa kujenga nyumba 32,000 pamoja na wa kubadili maji ya chumvi yawe salama kwa matumizi ya nyumbani.

Ingawa tayari kandarasi za mradi wa nyumba zilitolewa pamoja na maji kuvutia washirika wa kimataifa, bado haijang’oa nanga, ilhali amesalia na miaka miwili uongozini.

Katika Ruwaza ya Mwaka 2035 ya kaunti, Bw Joho aliahidi kuwa miradi hiyo ingeanza 2016, jambo ambalo lingali kwa makaratasi tu.

Baadhi ya miradi hiyo ambayo ilitarajiwa kugeuza na kuipa kaunti ya Mombasa sura mpya na pia kuiendeleza kiuchumi, ni pamoja na kujengwa kwa kiwanda cha kuuunda bidhaa mpya kwa kutumia taka ambacho kingegharimu Sh6.5 bilioni. Alizungumzia kuhusu kiwanda cha kugeuza maji ya chumvi ya baharini kusafishwa na kuweza kufaa kwa matumizi ya nyumbani. Mradi hiyo ungegharimu Sh16 bilioni.

Pia, mradi wa kuboresha makazi na kuzinduliwa kwa uchukuzi wa BRT uliotarajiwa kugharimu Sh200 bilioni.

Kulingana na mipango ya awali ya serikali ya kaunti, miradi hii ilipaswa kutimia kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na ile ya kibinafsi.

Bw Joho alikuwa amesema angetafuta msaada wa fedha kutoka kwa washirika wa kimataifa kutoka sekta binafsi.

Washirika hao walitarajiwa kufadhili miradi hiyo ambayo ingeangazia ukosefu wa kazi, kukabiliana na tatizo la takataka, kutoa maji safi kwa wakazi na kuona kuwa sekta ya usafiri imeboreshwa.

Hata hivyo, uchunguzi wa ‘Taifa Leo’ ulibaini kuwa wakazi wa Mombasa bado wanaendelea kukabiliwa na mrundiko wa takataka, ukosefu wa maji safi na wanaishi katika nyumba duni.

Mradi uchukuzi na ule wa kiwanda cha kugeuza taka bado haijajadiliwa.

Mwaka wa 2018, serikali ya kaunti ilisema kuwa kampuni mbili za kimataifa; Almar Water Solutions kutoka Uhispania na Aqua Swiss kutoka Uswisi zilipewa zabuni ya kutengeneza kiwanda kikubwa cha kusafisha maji.

Almar Water Solutions ilipaswa kutengeneza kiwanda hicho katika sehemu ya Kaskazini ya kaunti huku Aqua Swiss ikiunda kiwanda kingine kidogo upande wa Likoni.

Kulingana na makubaliano, kampuni hizo mbili zilipaswa kuchora muundo wa viwanda hivyo, zijenge na kuviendesha kwa miaka 25 kabla ya kuvikabidhi kwa serikali ya kaunti.

Kaunti ilisema kuwa mradi huo ungechukua angalau miaka miwili tu kukamilike na ulifaa kuanza Juni 2019.

Mradi wa makazi bora ulipangiwa kuleta afueni kwa kujenga nyumba 30,000 ili za kale katika mitaa ya Khadija, Miritini, Changamwe, Tudor, Mzizima, Buxton, Likoni, Nyerere, Tom Mboya, na Kaa Chonjo zibomolewe.

Hata hivyo, akizungumza na ‘Taifa Leo’, msemaji wa kaunti, Bw Richard Chacha alisema kuwa gavana anapanga kuanza miradi kadhaa mwaka 2020.

Pia aliongeza kuwa ana matumaini ule wa makazi bora utazinduliwa hivi karibuni ambapo nyumba 32,000 zitajengwa.