Habari za Kaunti

Wakazi Mombasa kufaidi kupitia mradi wa treni

January 7th, 2024 1 min read

NA ANTHONY KITIMO

WAKAZI wa Mombasa mwaka huu, 2023 wataanza kupata hudumu za uchukuzi wa treni kutoka kituo kikuu cha gari moshi baada ya serikali kutoa Sh10 bilioni za kukamilisha ukarabati wa reli ya zamani inayounganisha reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Maritini.

Serikali pia imesuluhisha suala la ulipaji fidia kwa eneo la umbali wa kilomita 1.4 kwa kutoa Sh1.17 bilioni kuwapa makao mapya walioathiriwa na mradi huo.

Katibu wa Uchukuzi Mohammed Daghar amethibitisha kutolewa kwa fedha hizo zitakazokamilisha ukarabati wa reli ya zamani (MGR), vituo vinginevyo na kituo kikuu cha reli eneo la katikati mwa mji.

“Tumetenga Sh4.9 bilioni kwa minajili ya ukarabati wa barabara ya reli, Sh4.2 bilioni kwa ujenzi wa Kituo cha Reli cha Central na Sh1.07 bilioni za ulipaji fidia utakaoendeshwa na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC),” akasema Bw Daghar.

Katibu huyo wa Wizara alisema mradi huo, ambao umekamilika kwa kiwango cha asilimia 70, unalenga kuunganisha katikati mwa mji wa Mombasa na Maritini wenye umbali wa kilomita 15.

Aidha, unalenga kuwatia motisha wakazi kutumia treni ya SGR.