Habari Mseto

Wakazi Mombasa watisha kuishtaki serikali kwa kuwafungia

October 2nd, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

WAKAZI wa mtaa wa Old Town jijini Mombasa, wametishia kushtaki serikali kuu na ya kaunti kwa kuwafungia mtaani humo wakati wa janga la corona.

Kupitia kwa muungano wao, wakazi hao wamelalamika kuwa marufuku ya kuingia na kutoka iliyowekewa sehemu hiyo msimu huu wa corona ilikuwa ni dhuluma kwa haki zao.

Marufuku hiyo iliwekwa kuanzia Mei hadi Juni. baada ya serikali kutangaza kuwa eneo hilo lilikuwa mojawapo ya kitovu cha maradhi ya Covid-19, wakazi wengi waliposemekana kuambukizwa virusi hivyo.

Kwenye kikao cha wanahabari jana katika ngome ya Fort Jesus, viongozi wa muungano huo wa wakazi (OTRA), walisema wanataka maelezo zaidi kuhusu kwa nini marufuku hiyo ilistahili, na pia wapewe thibitisho kuhusu idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa OTRA, Mbwana Abdalla, alisema walifanya uchunguzi kivyao kwa siku nne wakishirikiana na mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Muhuri na Okoa Mombasa kuthibitisha kama kweli watu wengi walikuwa wameambukizwa virusi hivyo jinsi serikali ilivyodai.

“Tulichukua sampuli kutoka kwa nyumba 1,012 katika vijiji 10 vya Old Town, na tukathibitisha kuwa matokeo yetu yalitofautiana na madai ya serikali,” akasema Bw Abdalla.

Mmoja wa waanzilishi wa chama hicho, Ahmed Awadh alisema kuwa wakazi wa Old Town lazima wafidiwe kwa kufungiwa ndani ya nyumba zao kwa mwezi mmoja.

“Tulipokataa kupimwa corona, baadhi ya viongozi wetu walitutusi na kutuita wazembe na kututishia kuwa watatufungia majumbani kwetu. Hatukupimwa na walitimiza vitisho vya kuweka marufuku hiyo. Tulifungiwa kidhuluma,” akasema Bw Awadh.

Alisema sasa wakazi wanataka serikali isiwalipishe ushuru wakazi na wafanyabiashara wa Old Town kwa miaka mitatu au mitano hadi biashara zao zitakaporejelea hali ya kawaida, na uchumi wa eneo hilo urudi kama ilivyokuwa hapo awali.

Wiki iliyopita, mwenyekiti wa Muhuri, Khelef Khalifa pamoja na Bw Abdalla, waliwasilisha ombi kwa Seneti wakitaka iiagize kaunti kueleza kuhusu njia walizotumia kuamua mtaa huo ulikuwa na idadi kubwa ya maambukizi.

Pia, waliiomba Seneti iagize kaunti kuwarejeshea pesa watu waliolipia huduma za karantini, wakazi wafidiwe kwa kupoteza ajira na waagize viongozi wa serikali wakutane na wakazi ili kutatua mvutano kuhusu masuala hayo.