Wakazi sasa wataka daraja liwekwe kivuli kuzuia jua

Wakazi sasa wataka daraja liwekwe kivuli kuzuia jua

Na MOHAMED AHMED

SIKU moja baada ya daraja la kuelea la Likoni kufunguliwa kwa umma, baadhi ya wakazi wa Mombasa wametoa wito kwa serikali kuweka kivuli kwenye daraja hilo.

Hii ni kufuatia hali ya anga ambayo inashuhudiwa muda mwingi eneo hilo la Pwani ambayo ni jua kali.

Wakazi hao walisema kuwa kivuli hicho pia kitasaidia kuwaziba wakati wa mvua wanapotembea kwenye daraja hilo la kilomita 1.2.

“Tuna furaha kupatiwa njia mbadala ya kutumia kuvuka eneo hili. Hii ni afueni kwetu lakini kama unavyoona kuna jua kali sana na daraja ni refu mno. Tunashukuru kwa mradi huu lakini kukiwekwa kivuli itakuwa bora kwa matumizi,” akasema Bw Ali Khamis, mkazi wa Peleleza.

Mkazi mwengine Joseph Shizama alisema kuwa wakati wa mvua nyingi itakuwa vigumu kutumia daraja hilo iwapo kivuli hicho hakitakuwepo.

Mbali na hilo, Bw Shizama alisema kuwa kwa asilimia kubwa daraja hilo litawasaidia pakubwa kwani kwa muda wamekuwa wakipata shida katika kivuko cha Likoni ambapo watu wanavuka kwa kutumia feri.

“Tunashukuru sana kwa mradi huu. Tumekuwa tukipata shida kwa sababu ya feri. Tunachukua muda mwingi sana. Leo nimetumia daraja hili na nimevuka kwa haraka mno. Huu ni mradi ambao utatusaidia sana,” akasema Bw Shizama.

Daraja hilo lilifunguliwa rasmi tarehe 1 mwezi huu kama ilivyoagizwa na Rais Uhuru Kenyatta baada ya ufunguzi rasmi wa mradi huo mwezi uliopita.

Mnamo Ijumaa wakati daraja hilo lilipofunguliwa wakazi pamoja na Wakenya wengine kutoka sehemu tofauti za nchi walifika kujionea na kuvuka kivuko cha Likoni wakitumia daraja hilo ambalo limejengwa kwa gharama ya Sh1.9 bilioni.

Mwandishi huyu pia alivuka kutumia daraja hilo na kuchukua dakika kumi kutoka upande mmoja hadi mwingine.

Daraja hilo linaanza eneo la Liwatoni upande wa Mombasa na kuishia eneo la Ras Bofu upande wa Likoni.

Caroline Wachira mkazi wa Nairobi alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutumia daraja hilo.

“Mimi nimetalii tu eneo hili na nimekaa Mombasa ili kusubiri tu lifunguliwe ndio na mimi nijaribu kuvuka. Nimefurahi sana kutumia daraja hili,” akasema.

Katika daraja hilo watoto pia walionekana kufurahia kutembea kutoka upande mmoja hadi mwengine.

You can share this post!

Wapiganaji waua 25 DRC mkesha wa mwaka mpya

Wito shule ziajiri walinzi wenye tajriba kuhakikisha...