Habari Mseto

Wakazi wa baadhi ya vijiji Lamu walazimika kutumia maji ya chumvi

December 5th, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

UHABA wa maji umewasukuma wakazi wapatao 600 wa vijiji vya Kiangwe na Mararani, Kaunti ya Lamu kutumia maji ya chumvi kutoka kwa Bahari Hindi kwa matumizi ya nyumbani.

Wakazi hao ambao vijiji vyao vinapatikana ndani ya msitu wa Boni wanasema kwa miaka mingi wamekuwa wakihangaika kwa kukosa maji safi ya kunywa, hali ambayo inawalazimu kutembea masafa marefu wakitafuta bidhaa hiyo.

Wanasema mara nyingi wamelazimika kuchota maji ya chumvi kutoka kwa Bahari Hindi kwa matumizi yao ya nyumbani hasa nyakati ambapo visima wanavyotegemea vinapokauka kufuatia kiangazi ambacho hushuhidiwa maeneo hayo mara kwa mara.

Msemaji wa akina mama katika kijiji cha Kiangwe, Bi Fatma Shizo, alisema wanawake ndio wanaohangaika zaidi kwani hulazimika kutembea kwa miguu kwa zaidi ya kilomita 30 wakitafuta maji visimani.

Mkazi wa Kiangwe, Kaunti ya Lamu, Bi Fatma Shizo aitaka serikali na wahisani kujitokeza kuwaanzishia mradi wa kusafisha maji kwa matumizi ya nyumbani ili kumaliza tatizo la maji eneo hilo. Picha/ Kalume Kazungu

Bi Shizo aliitaka serikali ya kaunti na wahisani kujitokeza na kuwajengea kituo cha kusafisha maji ya chumvi ili kuyageuza kuwasafi kwa matumizi ya binadamu kwenye eneo lao la Kiangwe.

“Maji ni tatizo kubwa hapa Kiangwe. Tunategemea maji ya mvua peke yake. Yakiisha tunalazimika kuingia msituni kuchimba visima ili kutafuta maji. Visima vingi ni vya maji ya chumvi, hivyo kupata kisima cha maji safi huwa ni vile vya sehemu ya mbali. Mara nyingi inatubidi kutumia haya maji ya Bahari Hindi ambayo ni ya chumvi. Tunachemsha na kisha kutumia kuoga au kutekelezea majukumu mengine nyumbani. Tunahofia huenda hali hiyo ikatusababishia maradhi,” akasema Bi Shizo.

Uhai

Bi Khadija Hussein alisema wanawake wengi katika vijiji vyenyewe wamekuwa wakihatarisha uhai wao kuingia msituni kutafuta maji ya visima vilivyoko huko.

“Msitu wa Boni una wanyama hatari na tunalazimika kuingia ndani na watoto wetu kutafuta maji ya visima. Serikali ituangalie kwa kuanzisha mradi wa kusafisha haya maji ya bahari yawe safi kwa matumizi ya nyumbani,” akasema Bi Husssein.

Katika kijiji cha Mararani, wakazi wanasema mara nyingi wamelazimika kukaa bila maji.

Wakazi aidha waliwashukuru maafisa wa usalama, ikiwemo wanajeshi wa KDF na polisi wanaohudumu eneo hilo kwa kuwa na mohyo wa ukarimu kwani wamekuwa wakiwasaidia wakazi hao kwa maji.

Bw Abdi Chengele alisema ipo haja ya serikali ya kaunti kuendeleza mpango wa kusambazia wakazi maji wakitumia malori.

“Hizi kambi za jeshi na polisi mara nyingi zimekuwa kiokozi chetu. Mara nyingi wanatusaidia kwa maji ya kunywa. Kaunti ilikuwa na mpango wa kusambaza maji vijijini kwa kutumia magari. Mpango huo uendelezwe kwani ni msaada mkubwa kwetu,” akasema Bw Chengele.