Wakazi wa Garashi wahimizwa kujenga vyoo

Wakazi wa Garashi wahimizwa kujenga vyoo

NA ALEX KALAMA

WAKAZI wa wadi ya Garashi katika eneobunge la Magarini kaunti ya Kilifi wamehimizwa kuzingatia usafi ili kujikinga na maradhi ya kuharisha yaliyokithiri eneo hilo.

Kulingana na afisa wa afya katika zahanati ya Karimboni eneo hilo Silas Bashora, idadi kubwa ya wagonjwa wanaozuru hospitali hiyo huwa wanaugua maradhi hayo.

Bashora aidha anadai kuwa hali hiyo imekuwa ikichangiwa na utumizi wa maji chafu hatua ambayo imewalazimu wahudumu wa afya kuielimisha jamii ya eneo hilo kuhusu jinsi ya kutibu maji ya kunywa.

“Watu wengi wakija hapa wako na shida ya kuharamisha tunajaribu kudhibiti huo ugonjwa, japo tunaendelea kuelimisha jamii kwamba uchafu si mzuri. Kama ni maji tunawaelimisha wayachemshe kwanza kabla ya kunywa ama waweke kama hizi dawa zetu water guard. Kwa sababu ugonjwa wa kuharisha unasababishwa na uchafu viini ambavyo vinapatikana katika maji yetu,” alisema Bw Bashora.

Wakati huo huo afisa huyo wa afya amewahimiza wakaazi wa eneo hilo kulipa kipaumbele swala la ujenzi wa vyoo ili kupunguza athari za maradhi hayo.

Vile vile Bashora ameiomba serikali ya kaunti hiyo kupitia idara ya afya kuweka mikakati ya kuboresha afya ya wakazi wanaoishi mashinani ili kudhibiti maradhi hayo.

“Uchafu mwingi unasababishwa na kutokuwa na vyoo. Wanajamii wajenge vyoo ili huu ugonjwa angalau hata kama hatutaweza kuudhibiti asilimia mia moja lakini uweze kupungua. Kwa serikali ya kaunti tujaribu kupunguza huu mkurupuko wa ugonjwa wa kuharisha katika hili eneo la Karimboni. Isitoshe, watu wengi wanakunywa maji ya mtoni ambayo si salama,” alisema Bw Bashora.

  • Tags

You can share this post!

Omanyala sasa alenga dhahabu ya Riadha za Dunia 2023 na...

Bandari: Azimio, KK wakwaruzana

T L