Habari Mseto

Wakazi wa Gatuanyaga waambiwa kila kitu tayari ujenzi wa barabara nzuri uanze

October 24th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Gatuanyaga katika Kaunti ya Kiambu sasa wanatarajiwa kuanza kutumia barabara nzuri.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema Jumatano wakazi hao watapata barabara ya kiwango cha Bitumen na itakuwa ya umbali wa kilomita 24.

Halmashauri ya ujenzi wa barabara za maeneo ya mijini – KURA – itajenga barabara ya Muguga-Ngirai-Munyu-Githima-Kang’oki-Kisii, halafu irudi hadi barabara kuu ya Garissa.

Akizungumza na wakazi wa Gatuanyaga, Bw Wainaina aliwahimiza watoe maoni yao bila kuogopa kuhusu jinsi ambavyo wangetaka ujenzi huo uendeshwe.

“Kila mmoja wenu ana nafasi ya kujieleza na ndiyo maana leo tuko hapa,” alisema mbunge huyo.

Alisema serikali imefanya jambo la kupongezwa kwa sababu tangu uhuru kupatikana barabara ya lami haijaonekana eneo hilo.

Kulingana na KURA uzinduzi wa ujenzi rasmi wa barabara hiyo ni Novemba 2020, ambapo itakamilika kwa muda wa chini ya miezi 30.

Wakazi wa eneo hilo waliridhika na uamuzi huo wa ujenzi huo huku wakisema ni mwamko mpya.

Hata hivyo wakazi wanaoishi karibu na sehemu kutakapojengwa barabara hiyo wameombwa kuhama mapema kabla ya kazi hiyo kuanza rasmi.

KURA imehimizwa kufanya juhudi kuona ya kwamba vijana wanaotoka sehemu hizo wanapata ajira wakati wa kazi hiyo ikiendelea.

“Tungetaka kuona vijana wetu wakiajiriwa wakati wa ujenzi huo badala ya kutafuta watu kutoka maeneo mengine,” alisema Bw Wainaina.

Wakati huo pia serikali imetenga Sh700 milioni zitakazotumika kukarabati barabara zilizoko katikati mwa mji wa Thika.

Wakazi hao walisema msimu wa mvua biashara nyingi husimama kwa sababu barabara nyingi huwa mbovu na kwa hivyo usafirishaji wa bidhaa huwa balaa.

“Sisi wakazi wa hapa tunafurahia juhudi za serikali kutuletea barabara maeneo haya. Tuna imani hali ya maisha itabadilika,” alisema Joseph Mwangi ambaye ni mkazi wa Gatuanyaga.