Wakazi wa Gatundu Kaskazini wataka walipwe fidia

Wakazi wa Gatundu Kaskazini wataka walipwe fidia

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Gatundu Kaskazini waliandamana mnamo Jumanne hadi katika bwawa la Kariminu wakitaka walipwe kiasi cha fedha walizoahidiwa baada ya kuhamishwa kutoka sehemu iliyokuwa makazi yao.

Kazi ya kila mara ya kuchimba bwawa hilo ilisitishwa kwa muda baada ya wakazi hao kufurusha mkandarasi na madereva wa matingatinga yaliyopo eneo hilo.

Maafisa wa polisi walifika eneo hilo kusitisha maandamano hayo huku wakazi hao waliokuwa na hasira wakiendelea kupiga kambi mahali hapo.

Wakazi hao wanadai kuwa kabla ya kuhama kutoka sehemu hiyo, waliahidiwa kuwa wangelipwa takribani Sh2.2 bilioni kama fidia ili wahamie kwingineko.

Walilalamika kwa ukali wakidai ya kwamba kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa wameishi maisha magumu ajabu huku wakishindwa wamlilie nani.

Walisema juhudi zao za kutafuta kukutana na viongozi wao ili wajitetee zimegonga mwamba bila matokeo mema.

Bw Kamau Gathanji wa kijiji cha Kanyoni, alisema kwa mwaka mmoja sasa wamepata shida kubwa na familia zao huku wakibaki kuwa ombaomba.

“Hata viongozi tuliotegemea wangetusaidia tayari wametuacha pekee yetu tujisaidie wenyewe. Sasa tunamwomba Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati kuona ya kwamba mambo yetu yanatatuliwa haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Gathanji.

Alisema wao havana shida na kuendelea kwa mradi huo lakini shida yao kuu ni kuona ya kwamba wanalipwa haki yao haraka iwezekanavyo ili waendelee na maisha yao ya kawaida.

Bi Alice Nduta wa kijiji cha Gathanji akasema wamebaki maskini wasio na mbele wala nyuma.

Alisema hawana mashamba ya kulima na kwa hivyo wamebaki pweke bila kujua watafanya nini hapo baadaye.

Akaongeza pia hata watoto wao wengi wanatatizika kuhudhuria shule.

“Sisi kama wakazi wa hapa Gatundu tunaiomba serikali ifanye hima kuona ya kwamba inatujali ili tuweze kuendelea na maisha jinsi hali ilivyokuwa hapo awali.

Alizidi kueleza kuwa wakati huu mvua inazidi kunyesha na wamekuwa katika hali ngumu ya maisha.

“Wakati kama huu ndipo maradhi mengi hupatikana na kwa hivyo serikali ichukue hatua ya haraka ili ituokoe kutoka kwa maisha magumu,” alijitetea Bi Nduta.

You can share this post!

Faida za kula malenge

Wakulima wa Mataara wapinga uchaguzi wa ghafla