Habari

Wakazi wa Giciiki Thika Magharibi wahama kufuatia mafuriko

December 5th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Giciiki katika eneo la Gatuanyaga, Thika Mashariki, wamelazimika kuhama kutoka makazi yao kufuatia mvua iliyopitiliza inayoendelea kunyesha kote nchini.

Waliozungumza na Taifa Leo wamesema kwa muda wa wiki moja sasa maji yatokanayo na mvua yamewakosesha amani katika makazi yao huku wakilazimika kutafuta maeneo salama.

Walisema karibu kila msimu ifikapo wakati wa mvua maisha yao huwa katika hali ya hatari wasijue la kufanya kutokana na mafuriko ya mvua.

Mwenyekiti wa Maslahi ya Wanaume wa Giciiki – Gaciiki Men Welfare Association – Bw Simon Ngige amesema kuna mtaro mkubwa ambao hubeba maji mengi sana kunaponyesha, na hivyo husababisha kusambazwa kwa maji mengi katika mashamba yao na makazi.

Amesema mashamba makubwa yaliyoko katika eneo hilo yamefurika maji ya mvua ambapo “eneo lote limegeuka mto.”

“Sisi wakazi wa eneo hili hatuna jambo la kufanya kwa wakati huu kwa sababu kila mmoja anahama na mizigo yake ili kutafuta mahali salama pa kuishi. Hata wengi wa wakazi walianza kuhama jana Jumatano kwa kuhofia uhai wao. Ni hatari kwetu kwa sababu wengi wamelala katika baridi ya usiku,” amesema Bw Ngige.

Wakazi hao wamesema wanahofia maradhi hatari yanaweza kuwavamia wakati wowote ule, na kwa hivyo wanaiomba serikali kupitia mbunge wao Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina kuingilia kati ili kuona ya kwamba wanapata vifaa muhimu vinavyoweza kuwasaidia.

“Kwa sasa hatuma mbele wala nyuma na cha muhimu ni wahisani wajitokeze ili kutusaidia sisi wakazi wa Giciiki ambao wengi wetu hatuna uwezo wa kifedha,” amesema Bw Ngige.

Eneo la makazi Gaciiki ambako kumejaa maji ya mafuriko. Picha/ Lawrence Ongaro

Mwaka 2018 pia kulinyesha mvua iliyosababisha kadhia ambapo ilibidi wakazi wengi kuhama kwa wiki chache kabla ya kurejea katika makazi yao.

“Kile kinachotupa hofu ni kwamba wanawake wenye watoto wachanga wako katika hali mbaya hata wasijue la kufanya. Hata tunahofia sana kama watoto wetu watarejea shuleni muhula wa kwanza wa mwaka 2020 shule zitakapofunguliwa,” amesema Bw Ngige.

Amesema hata usafiri umekuwa shida kubwa ambapo magari na hata pikipiki za wahudumu wa bodaboda zinashindwa kufika karibu na eneo hilo huku ikionekana kuwa wakazi hao hawana jinsi ya kusafiri kutekeleza shughuli zao za kawaida.

Wakazi hao wanasema cha muhimu kwa sasa ni kutafuta namna ya kupata chakula kwa sababu mambo yakiendelea hivyo bila shaka njaa italeta hasara kubwa na huenda ikasababisha afya zao kuzorota.

Kwa sasa wakazi wengi wameacha shughuli zao za kawaida na kuendelea kutafuta hifadhi mahali pema karibu na makazi yao.

“Kwa wakati huu akili zetu zinawazia kupata makazi salama, kupata chakula, na kulinda afya zetu,” amesema mkazi mmoja ambaye hakujitambulisha.