Habari Mseto

Wakazi wa Gituamba eneobunge la Gatundu Kaskazini waandamana kulalamikia ubovu wa barabara

November 1st, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

SHUGHULI za uchukuzi katika barabara ya Gatukuyu kuelekea Mataara zilitatizika baada ya wakazi wa Gituamba kufanya maandamano.

Wakazi hao mnamo Alhamisi walitembea kilomita kadha wakionyesha ghadhabu yao jinsi barabara hiyo ya kilomita 30 iliyokuwa bovu kupita kiasi.

Kulingana na wakazi hao watu wengi walioathirika na barabara hiyo ni wafanyi biashara na wana bodaboda ambao wamepitia masaibu mengi sana.

Wakati wa maandamano hayo usafiri ukilisitishwa kwa muda ili wakazi hao waonyeshe jinsi walivyokerwa na jambo hilo.

Mkazi mmoja ambaye hakujitambulisha alisema kwa muda mrefu wamekuwa na shida ya usafiri huku viongozi wakishindwa kuingilia kati.

“Sisi kama wakazi wa hapa leo tumekusanyika eneo hili la Gituamba ili kutoa malalamiko yetu kuhusu jinsi barabara ni bovu,” alisema mkazi huyo na kuongeza hawatakubali viongozi kuwahadaa hivyo huku wakazi wakiumia hivyo.

Mhudumu wa bodaboda wa Gituamba, Bw Muniu Kayuni alisema pikipiki zao zimekuwa zikitenda ajali kila mara kwa kuteleza kwa matope.

“Mara nyingi unapata ya kwamba pikipiki inateleza na kuanguka huku mteja uliyembeba pengine akivunjika miguu. Na katika hali hiyo, utalazimika kumpeleka hospitalini,” alisema Bw Kayuni.

Alisema katika eneo la Gatundu Kaskazini hakuna maendeleo ya kuridhisha ukilinganisha na Gatundu ya Kusini.

“Sisi kama wakazi wa eneo hili la Kaskazini tungetaka mambo yetu pia yaangaziwe kama maeneo mengine,” alisema Bw Kayuni.

Mkazi mwingine Bw Peter Karanja alisema mara kadha wameahidiwa maendeleo lakini bado hakuna cha muhimu cha kujivunia kama wakazi wa Gituamba.

Alisema aliyepewa kandarasi hiyo anastahili kufurushwa na mwingine mwenye ujuzi kamili akamilishe kazi hiyo ya barabara.

Alizidi kueleza ya kwamba wale walioathirika zaidi katika hali hiyo ni wafanyabiashara na wahudumu wa bodaboda ambao kazi yao hutegemea barabara hiyo.